1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran ikisistiza juu ya haki yake ya kuongeza uzalishaji.

Sylvia Mwehozi2 Juni 2016

Saudi Arabia imeahidi kwamba haitazidisha uzalishaji wa mafuta katika soko, wakati ambapo nchi wazalishaji wa mafuta wa jumuiya ya OPEC wakianza mjadala mzito unaohusu sera za uzalishaji wa mafuta huko mjini Vienna.

https://p.dw.com/p/1Izbe
Österreich Wien OPEC Meeting
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Zak

Saudi Arabia imeahidi kwamba haitazidisha uzalishaji wa mafuta kwa kuongeza mapipa ya ziada katika soko, wakati ambapo nchi wazalishaji wa mafuta wa jumuiya ya OPEC wakianza mjadala mzito unaohusu sera za uzalishaji wa mafuta huko mjini Vienna, huku Iran ikisistiza juu ya haki yake ya kuongeza uzalishaji.

Mvutano baina ya taifa la kifalme la Kisunni na Jamhuri ya Kiislamu inayoongozwa na washia, umekuwa ni ajenda muhimu katika mikutano iliyopita ya nchi wazalishaji wa jumuiya ya OPEC, ikiwemo ule wa mwezi Disemba 2015 wakati kundi hilo liliposhindwa kukubaliana juu ya lengo rasmi la matokeo ya pamoja kwa mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa.

Vyanzo kadhaa vya OPEC vinasema kwamba Saudi Arabia na washirika wake wa nchi za Ghuba wanapendekeza kuwepo na kiwango cha pamoja cha ukomo wa juu katika jaribio la kutaka kukarabati umuhimu wa OPEC na kuhitimisha vita ya soko la pamoja ambayo imeathiri bei ya mafuta na kupunguza uwekezaji.

Kushindwa kufikia makubaliano yoyote kutafufua hofu juu ya soko ambapo Saudi Arabia kama mzalishaji mkubwa ndani ya OPEC tayari ina rekodi za juu na inaweza kuongeza uzalishaji utakaowaadhibu wapinzani wake na kujikuta ikipata soko la ziada. Waziri mpya wa mafuta wa Saudi Arabia Khalid al-Falih amewaambia waandishi wa habari kuwa.

"Kama kuna uhaba katika soko kwa sababu yoyote ile, Saudi Arabia itahitajika kukidhi mahitaji ya uchumi wa dunia na wateja wetu.Tutafanya tuwezalo, siwezi kuyataja kama ni mafuriko, tutasambaza mafuta kama kuna haja katika soko la mafuta." amesema waziri huyo.

Saudi Arabia inalalamikiwa kwa kuzalisha mafuta zaidi ya kiwango kilichoainishwa na hivyo kulifanya soko la mafuta duniani kukumbwa na mshtuko wa uzalishaji mafuta ya ziada kuliko mahitaji.

Alipoulizwa ikiwa nchi yake itapendekeza kuwepo kwa njia za matokeo ya pamoja, waziri Al-Falih amesema kwamba watafanya kila lililokuwa na umuhimu akiongeza kwamba itategemea na nini Iran ataweka mezani.

Waziri wa mafuta wa Iran Bijan Zangeneh
Waziri wa mafuta wa Iran Bijan ZangenehPicha: Reuters/Bader

Makubaliano yoyote baina ya Riyadh na Tehran yanaweza kuwa ni mshangao katika soko la mafuta , ambapo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kumeonekana ongezeko la mapigano baina ya maadui wa kisiasa wanaopigana vita nchini Syria na Yemen.

Iran imekuwa kikwazo kikubwa katika ukanda wa nchi wazalishaji wa mafuta, katika kukubaliana juu ya sera ya mapato katika kipindi cha miaka kadhaa sasa wakati huo ikiongeza usambazaji wa mafuta licha ya wito kutoka kwa wanachama wengine wa wa kufungia uzalishaji.

Inataka iruhusiwe kuongeza uzalishaji katika kiwango kinachoonekana kwa hivi sasa baada ya kumalizika kwa vikwazo vya magharibi juu ya mpango wake wa Nyuklia.

Waziri wa mafuta wa Iran, Bijan zanganeh anasema Tehran haitaunga mkono njia za matokeo ya pamoja na kwamba mjadala huo ujikite katika soko la mafuta kulingana na a uwezo wa nchi wa kuzalisha mafuta.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/reuters

Mhariri:Iddi Ssessanga