1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa uchumi Afrika wamalizika.

Sekione Kitojo15 Juni 2007

Viongozi wa kisiasa na biashara wanaohudhuria mkutano wa kila mwaka wenye lengo la kuleta mwelekeo ya wafanyabiashara katika bara la Afrika wameisifu China na India kwa kiu yao kubwa ya kupata mali ghafi , kuwa italeta msukumu mkubwa wa kunyanyua uchumi wa bara la Afrika kwa kiasi fulani.

https://p.dw.com/p/CB3Y

Katika mkutano huo wa mkutano wa dunia juu ya uchumi wa Afrika ambao umemalizika leo , hata hivyo majadiliano yamegubikwa na suala ambalo linajadiliwa sana hivi sasa , kuwa mataifa hayo mawili, China na India yanaweza kuiacha Afrika mikono mitupu baada ya kunyakua mali yote ya asili waitakayo.

China inapata soko kubwa katika bara la Afrika kwa bidhaa zake ambazo ni rahisi. Na mataifa yenye utajiri mkubwa wa mafuta kama vile Nigeria na Angola yanaitatia nchi hiyo maliasili hiyo ambayo inahitajiwa sana na China ili kuuendeleza uchumi wake unaokua kwa haraka.

Katika kikao cha mwisho leo Ijumaa rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki amesema kuwa tatizo moja kubwa kabisa lilikuwa ni kujaribu kuligawa bara la Afrika katika sehemu ndogo ndogo zenye mataifa 53 tofauti kwa kuweka vizuizi vya kibiashara dhidi ya bidhaa kutoka nchi nyingine.

Kila mmoja amesema anatambua umuhimu wa kuondoa vizuizi hivyo miongoni mwetu.

Changamoto lakini ni kuweza kufanikisha suala hilo, ameongeza rais Mbeki.

Mataifa makubwa manne yenye nguvu kubwa za kiuchumi katika bara la Afrika yanaweza kuwa ingini ya ukuaji wa kimkoa katika njia ile ile ambayo masoko yanayokua kama vile Brazil , Russia, India na China yamekuwa mfano katika eneo lote la mataifa yanayoendelea duniani, mtafiti mwandamizi katika benki ya maendeleo ya Afrika amesema.

Afrika kusini, Algeria, Nigeria na Misr zinatoa kiasi cha jumla cha zaidi ya nusu ya pato jumla la kila mwaka la Afrika , yakijiweka mataifa hayo pamoja na Brazil , Russia, India na China mataifa ambayo yanaathari katika masoko ya maeneo yao ya kimkoa.

Inaeleweka bila shaka , kuwa mataifa hayo yenye uchumi wenye nguvu katika bara la Afrika yanayojulikana kama SANE ,yanaonekana zaidi katika utajiri wa Afrika , amesema Temitope Oshikoya, mkurugenzi wa utafiti wa maendeleo katika benki ya maendeleo ya Afrika.

Ametoa mifano kadha ya uwezo wa mataifa hayo kuleta athiri kwa mataifa mengine, kama vile uwezo wao wa kutumia kundi kubwa la wafanyakazi, na kuhimiza biashara miongoni mwa mataifa ya Afrika.

China , Russia, India na Brazil zinafanya nguvu kuu kama kundi katika uchumi wa dunia . Kile ambacho kinahitajika hivi sasa kwa kweli ni kuhakikisha uratibu sahihi miongoni mwa mataifa haya manne ya Afrika , ili kuweza kuzungumza kwa sauti moja kwa niaba ya Afrika duniani na katika kiwango cha kimkoa.