1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Ulaya na Afrika waanza Brussels

Admin.WagnerD2 Aprili 2014

Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika unaanza leo katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels, ukihudhuriwa na wakuu wa nchi na serikali wapatao 70 kutoka Ulaya na Afrika.

https://p.dw.com/p/1Ba24
Rais Paul Kagame wa Rwanda na Waszir wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza William Hague mjini Brussels
Rais Paul Kagame wa Rwanda na Waszir wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza William Hague mjini BrusselsPicha: Reuters

Kuitishwa kwa mkutano huu wa nne kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika kuligubikwa na miito ya kuususia kutokana na kutoalikwa baadhi ya nchi, kama vile Sudan ambayo rais wake Omar al-Bashir anakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, na Zimbabwe, ambako mke wa rais Robert Mugabe amewekewa vikwazo vya usafiri. Hata hivyo inatarajiwa kwamba viongozi wa mataifa 40 ya kiafrika watahudhuria mkutano huo ambao unafunguliwa rasmi mchana wa leo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye ni mmoja wa viongozi watakaoshiriki, amesema ushirikiano kati ya Ulaya na Afrika ni muhimu kwa maendeleo ya pande hizo mbili.

Mwanzo mpya wa uhusiano

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy amesema anayo matumaini mkutano huu utakuwa mwanzo mpya wa uhusiano kati ya Ulaya na Afrika, na kuongeza kuwa Ulaya inayo maslahi makubwa katika kuhakikisha kwamba Afrika inakuwa na amani na maendeleo, na kuwa sehemu ambako haki za watu wote zinaheshimiwa.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van RompuyPicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza leo kabla ya kuanza mkutano huo, rais wa Halmashauri kuu ya Ulaya Jose Manuel Barroso amesema mnamo miaka mitatu ijayo, Umoja wa Ulaya utatoa kiasi cha Euro milioni 800, kusaidia mradi wa pamoja baina ya Umoja huo na Afrika katika kuzuia mizozo.

Hata hivyo, rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf amesema hatua bora ambayo Ulaya yaweza kuichukua kusaidia bara la Afrika ni kusaidia kukua kwa uchumi wake.

''Natumai kwamba nchi za Ulaya, ambazo nyingi ni wadau wa Benki ya Afrika ya Maendeleo, zitaiunga mkono ipasavyo benki hiyo. Kwa sababu muhimu zaidi sio kuzinusuru nchi dhaifu katika mizozo, bali kuzisaidia nchi zote kujiimarisha, ili ziweze kukabiliana na mizozo hiyo inapoibuka.'' Amesema rais Sirleaf Johnson.

Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf
Rais wa Liberia Ellen Johnson SirleafPicha: Getty Images

Haki za binadamu kuangaziwa

Masuala mengine muhumu yanayotarajiwa kuwepo kwenye meza ya mkutano huo kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika ni yale yahusuyo mabadiliko ya tabia nchi, umasikini, uhamiaji na haki za binadamu, hususan kufuatia hatua ya Uganda kupitisha sheria dhidi ya ushoga, ambayo imekosolewa sana na washirika wake wa nchi za magharibi. Edmundo Matos kutoka chama tawala nchini Msumbiji, FRELIMO, amesema itabidi Ulaya ikubali ukweli kwambaAfrika inavyo vigezo vyake vya maadili ya jamii.

Rais Catherine Samba Panza na Katibu Mkuu Bani Ki-moon
Rais Catherine Samba Panza na Katibu Mkuu Bani Ki-moonPicha: Reuters

Pembeni mwa mkutano huu kitafanyika kikao maalum kujadili hali inayojiri katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambacho kitamshirikisha rais wa mpito wa nchi hiyo Catherine Samba Panza, na viongozi wa nchi ambazo zinashiriki kwa kiwango kikubwa katika kurejesha amani na kutoa msaada wa kibinadamu katika nchi hiyo.

Jana, Umoja wa Ulaya ulitangaza kuwa unaanzisha ujumbe wake wa amani katika nchi hiyo, ambao umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu. Ujumbe huo utawashirikisha wanajeshi 1000, ambao watakwenda kuwaunga mkono wanajeshi wa Ufaransa na wa Umoja wa Afrika ambao tayari wanajaribu kutuliza mgogoro wa umwagaji damu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DPAE/AFPE

Mhariri:Yusuf Saumu