1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Uhaianuai

Miraji Othman19 Mei 2008

Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya uhaianuai, yaani uhusiano wa kimaumbile kati ya mimea na viumbe, ulianza leo mjini Bonn, hapa Ujerumani

https://p.dw.com/p/E2aa
Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya uhaianuai mjini Bonn, UjerumaniPicha: AP


Mkutano huo unaohudhuriwa na watu 6,000 kutoka nchi 191, kwa hakika, sio kongamano la taaluma ya sayansi, lakini ni mkusanyiko wa kisiasa. Mbele kabisa katika mazungumzo haya ya wiki tatu ni suala la kuyalinda maumbilie, na hasa masharti ya kumwezesha mwanadamu aendelee kuishi hapa duniani. Kwani jambo moja ni wazi: bila ya maumbile hakuna maisha.



Juu ya umuhimu wa hali ya hewa kwa ajili ya maisha yetu hapa duniani ni jambo linaloeleweka na kila mtu duniani. Lakini suala la kulinda mimea na viumbe ni jambo lisilotambuliwa vya kutosha nje ya duru za wanasayansi. Hali hii inafaa na inabidi ibadilike. Kwani ulinzi wa kile mabingwa wanachokiita uhaianuai, hauhusu tu kulinda wanyama na mimema, lakini hasa kiini chake ni kuilinda idadi inayoongezeka ya wanadamu pamoja na vyakula vyao; vipi watu hao wanavoweza kupatiwa rasil mali na madawa ya kutosha na nani anayefaidika, kiuchumi, kutokana na madawa hayo. Sio tu ulinzi wa hali ya hewa ni jambo lenye umuhimu wa kimsingi kwa maisha ya hapa duniani, lakini sawa pia jambo hilo lina umuhimu kwa ulinzi wa mimea na viumbe.


Mkutano huu wa Bonn hasa utashughulikia namna ya kuutekeleza ule mkataba wa kulinda mimea na wanyama mbali mbali ambao ulikubaliwa mjini Rio de Janeiro katika mkutano wa kilele wa Dunia hapo mwaka 1992, na kutiwa saini na nchi 150, lakini bila ya Marekani. Kama ule mkataba wa dunia juu ya ulinzi wa hali ya hewa, Marekani ilifuata njia yake peke yake kuhusu mkataba wa kulinda mimea na viumbe. Kwa mujibu wa mkataba wa Rio ni kwamba rasil mali ya asili ya viumbe sio tena urithi wa mwanadamu, lakini wanyama, mimea, bakteria, vyote hivyo pamoja na habari zao ni urithi wa madola ambako vitu hivyo vinatokea. Hapo ndipo panapoanza mabishano juu ya kagawana faida pale, kwa mfano, katika sekta ya tiba kampuni la kimataifa la kutengeneza madawa linapchukuwa haki milki kamili ya maarifa na mimea ambayo imekuwa ikitumiwa katika sekta ya uganga kwa vizazi vingi kwenye nchi yenye kuendelea. Nchi zinazoendelea zinataka kushiriki katika kutumiwa rasili mali za asili ya viumbe na mimea ilioko katika nchi zao.


Hamna mtu anayeweza kuzilaumu nchi hizo zinazoendelea kwa kuendesha mapambano yao dhidi ya uharamia huo unaofanyiwa uhai wao. Na hapa pia kuna suala la upande wa kifedha katika kugawana faida; kwa mfano, kulinda aina mbali mbali za mimea na viumbe kwa kupitia njia za kuzuwia kuchafuliwa zaidi maumbile. Suala hilo limefungamana na fedha nyingi na pia maslahi yalio na nguvu, kwa mfano kulinda misitu mikubwa yenye mimea na viumbe mbali mbali. Pale misitu hiyo inapunguzwa, na juu ya ardhi hiyo kunapandwa mimea ambayo kutokana nayo tunaweza kujipatia mafuta. Na pindi misitu hiyo italindwa, mimea hiyo itachukuwa maeneo ya ardhi ya kilimo na kushindana na ardhi inayolimwa kwa ajili ya mazao ya vyakula kwa ajili ya binadamu na wanyama. Matokeo yake ni kwamba- ukitilia maanani pia kuengezeka idadi ya watu duniani- ni upungufu wa vyakula, jambo ambalo linasababisha kupanda bei za vyakula; hivyo watu walio maskini hawawezi kulipia. Suali: jee inabidi watu wengine wafe kwa njaa ili watu wengine waweze kuendesha magari yao? Hiyo ni moja ya mada zinazojadiliwa katika mkutano huu wa mjini Bonn. Licha ya hayo ni kwamba ulinzi wa misitu unafungamana na ulinzi wa viumbe na mimea pamoja na hali ya hewa.


Licha ya kwamba katika masuala haya ndani yake yako kuna maslahi ya kiuchumi yanayobishana, lakini mkutano huu unakubaliana katika lengo, lakini haukubaliani katika njia za kufikia lengo hilo. Hata hivyo, wakati unakwenda, kwani kwa mujibu wa maazimio ya mkutano wa kilele wa Dunia wa Rio inatakiwa kwamba hasara inayopatikana katika uhaianuai ipunguzwe sana ifikapo mwaka 2010. Katika mkutano ujao wa kilele huko Japan, miaka miwili kutoka sasa, inatarajiwa kutaamuliwa juu ya mkataba wa kimataifa utakaoilazimisha kila nchi ilinde uhaianuai. Na katika jambo hilo, nchi 190 zinazoshiriki katika mkutano wa sasa wa Bonn ziko mbali kufikia. Tatizo hasa ni kwamba nchi za viwanda hazitaki kubeba majukumu mepya ambayo yatazifaidia nchi zinazoendelea. Ulinzi wa viumbe na mimea sio jambo linaloweza kufikiwa bila ya gharama. Mapatano yatakayoweza kufanya kazi kikweli, na ambayo yatachangia kwa mwanadamu kuendelea kuishi yana bei yake. Lakini pia kutochukuwa dhamana na kutofanya lolote ni jambo ambalo litakuwa ghali baadae kwa mwanadamu. Uharibifu wa maumbile duniani unasababisha kila mwaka nakisi ya neema yenye thamani ya mabilioni kwa mabilioni ya dola.