1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa usalama mjini Munich

4 Februari 2013

Mkutano wa usalama mjini Munich,makubaliano ya biashara huru kati ya Ulaya na Marekani na sheria maalum za makosa ya jinai kwa wazee ni miongoni mwa mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/17XZZ
Washiriki katika mkutano wa usalama mjini MunichPicha: Reuters

Tuanzie lakini Munich ulikomalizika mkutano wa 49 wa usalama.Gazeti la "Landeszeitung" linaandika:"Mkutano wa kimataifa unastahiki sifa zake kama jukwaa la mizozo ya kimataifa. Hata hivyo matokeo yake mara nyingi yanakuwa finyu. Lakini safari hii kumechomoza matumaini ,pengine zikaanzishwa juhudi za kusaka ufumbuzi wa kisiasa pamoja na serikali ya Iran kuhusu mradi wake wa kinuklea. Matokeo hayo ni muhimu kwasababu wataalam wanaamini serikali ya Marekani huenda ikaamua mwaka huu tulio nao kuhusu vita au amani pamoja na Iran. Ingawa uwezekano wa kufikiwa ufumbuzi wa kisiasa ni mdogo kwasababu Teheran inafungamanisha mazungumzo ya ana kwa ana na kupunguzwa makali vikwazo vilivyoko, hata hivyo madhara ya kushindwa mazungumzo yatakuwa makubwa mno kwa namna ambayo hakuna atakaejiruhusu kuiachilia fursa hiyo ipite."

Uhusiano wa Marekani na Urusi

Sergey Lavrov und Joe Biden
Waziri wa mambo ya nchi za anje wa Urusi Sergey Lavrov na makamo wa rais wa Marekani Joe Biden katika mkutano wa Usalama mjini MunichPicha: Getty Images

Gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" linazungumzia mada zilizohodhi mkutano wa usalama mjini Munich na kuandika:"Munich inaendelea kuwa mahala pa makusudio.Katika mada sugu la Syria, misimamo imesalia vile vile-hakuna kilichobadilika na uhusiano ambao mtu anaweza kuutaja kuwa ni wa uadui kati ya Urusi na Marekani, ingawa ulijadiliwa lakini pia haukubadilika. Kila kitu kitategemea jinsi rais Barack Obama atakavyolenga siasa yake ya nje siku zijazo.Hata hivyo kuna kila sababu ya watu kujiwekea matumaini mema baada ya mkutano wa mjini Munich."

Ushirikiano wa kiuchumi

Gazeti la "Rheinpfalz "limeandika kuhusu makubaliano ya biashara huru kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani.Gazeti limeendelea kuandika:Makundi yanayopigania masilahi ya wakulima humu nchini yatajaribu kuyazuwia makubaliano ya biashara huru au "Tafta" kama wamarekani wanavyoyaita. Badala yake viwanda vya Marekani naiwe vya magari au vya uhandisi, vitaingiwa na hofu ya uhuru na mashindano ya kibiashara pamona na Ulaya. Ndio kusema kwa hivyo hakutokuwa na makubaliano ya Tafta? Marekani na ulaya wanabidi wajaribu kubuni soko la pamoja katika sekta nyingi na tofauti. Washirika wote wawili wanahitaji changamoto za aina mpya za kiuchumi. Na wakati ni muwafak hivi sasa kuanzisha jaribio kama hilo.

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu uwezekano wa kubuniwa sheria maalum za makosa ya jinai kwa wazee.Gazeti la "Mitteldeutsche Zeitung" linaandika:"Wataalam wanaohusiana na makosa ya jinai wameingiwa na wasi wasi hasa linapohusika suala la wazee. Kutokana na kuzidi kuongezeka idadi ya makosa ya jinai yanayofanywa na watu wenye umri mkubwa,wataalam hao wanashauri pawepo sheria maalum kuhusu wazee. Sheria ya makosa ya jinai kwa vijana wadogo ndio inayoangaliwa kama mfano wa kufuatwa. Lakini suala watu wanalojiuliza ni jee tunaelekea wapi, ikiwa siku za mbele sheria haitakuwa sawa kwa wote?"

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef