1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Usalama wa Kimataifa wamalizika Munich

P.Martin11 Februari 2008

Mkutano wa Usalama wa Kimataifa wa 44 umemalizika siku ya Jumapili katika mji wa Munich,kusini ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/D5a3
In a photo provided by the Security Conference Germany's Defense Minister Franz Josef Jung, left, welcomes US Defense Secretary Robert Gates, right, on the last day of the Conference on Security Policy in Munich, southern Germany, on Sunday morning, Feb. 10, 2008. (AP Photo/Security Conference, Sebastian Zwez, HO)
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung(shoto)na waziri mwenzake wa Marekani Robert Gates katika Mkutano wa Usalama wa Kimataifa mjini Munich,UjerumaniPicha: AP

Kwa mara nyingine tena,Waziri Ulinzi wa Marekani,Robert Gates sawa na baadhi ya viongozi wengine alionya juu ya hatari ya kutokea mgawanyiko katika NATO.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari,wanasiasa wa Ujerumani wanazingatia suala la kuongeza idadi ya vikosi vya Ujerumani nchini Afghanistan.Je,Ujerumani ndio imesalim amri kutokana na shinikizo la washirika wa NATO?Waziri wa Ulinzi wa Marekani,Robert Gates mjini Munich hakueleza moja kwa moja msimamo wake kuhusu fununu hizo.Lakini alieleza kinagaubaga kuwa Marekani haitazamii kazi za ukarabati tu kutoka washirika wake wa Ulaya nchini Afghanistan.

Mara kwa mara,wajumbe wa Marekani wamelalamika kuwa nchi shirika za Ulaya hazikufanikiwa hasa kuueleza umma umuhimu wa vita hivyo.Hata hivyo,Waziri Gates hakutaka kueleza ni kipi hasa anachokitaka kutoka washirika wa Ulaya hasa upande wa Ujerumani,ingawa siku chache zilizopita alituma barua kali kwa waziri wa ulinzi wa Ujerumani.Juu ya hivyo kwenye mkutano wa Munich,Gates alisifu kazi zinazotekelezwa na vikosi vya Ujerumani kaskazini mwa Afghanistan.Lakini kupelekwa kwa vikosi vya Ujerumani kusini mwa Afghanistan ni hatua iliyopingwa kabisa na Waziri wa Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier.

Hata hivyo,Marekani inaendelea kuwashinikiza washirika wake wa Ulaya kutoa msaada zaidi,si nchini Afghanistan tu bali hata kupiga vita ugaidi kote duniani.Waziri wa Ulinzi wa Marekani katika hotuba yake mwishoni mwa mkutano wa Munich alisema,wala yasiwepo matumaini kuwa hali ya mambo itabadilika duniani,pale serikali mpya itakaposhika madaraka Marekani kufuatia uchaguzi wa rais utakaofanywa mwezi wa Novemba nchini humo.Amesema,haidhuru chama gani kitashika madaraka-vitisho vya ugaidi vitaendelea kuwepo duniani.

Hiyo humaanisha kuwa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO itaendelea na majadiliano yake.Kama vile katika mkutano wa NATO utakaofanywa mwezi wa April katika mji wa Bucharest nchini Rumania.Katibu Mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer amekwisha tambua ukweli huo na amesema,mdahalo katika NATO ni jambo zuri kwa hivyo yeye anakaribisha utamaduni wa majadiliano na mabishano.