1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa mataifa ya Ulaya wakutana Prague

Tatu Karema
6 Oktoba 2022

Mkuu wa sera za kigeni wa EU Josep Borrell amesema viongozi 44 wa mataifa ya Ulaya wanakaokutana mjini Prague kwa mkutano wa uzinduzi wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya (EPC) watatuma ishara ya wazi ya kutengwa kwa Urusi

https://p.dw.com/p/4HpNm
EU Politiker Josep Borrell
Picha: Jean-Francois Badias/AP/dpa/picture alliance

Jumuiya hiyo ya EPC ambayo wazo la kuanzishwa kwake lilitolewa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, inayaleta pamoja mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya na mengine 17 yanayojumuisha mataifa kadhaa yanayosubiri kujiunga na Umoja huo na taifa la kipekee la kwanza kujiondoa katika Umoja huo, Uingereza. Borrell amesema kuwa mkutano huo ni njia ya kutafuta utaratibu mpya bila Urusi na haimaanishi kuwa wanataka kuitenga Urusi milele lakini kwamba Urusi ya Putin haina nafasi katika jumuiya hiyo.

Borrell asisitiza kujumuishwa kwa mataifa mengi

Borrell amesisitiza kuwa mkutano huo wa EPC ujumuishe nchi kutoka Uingereza kuelekea Serbia hadi Uturuki ikianzia Caucasus hadi bahari ya Kaskazini na bahari ya Mediterania. Mkutano huo wa Prague, unaonekana kuwa onesho la mshikamano kwa bara ambalo limekumbwa na migogoro mingi  ikiwa ni pamoja na athari za kiusalama na kiuchumi kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine. Hata hivyo, waandalizi wa mkutano huo bado hawajakuwa wazi kuhusu malengo muhimu ya kikao hicho.

Mnamo mkesha wa mkutano huo siku ya Jumatano, Borell alisema kuwa viongozi wengi wangekutana kwa nusu siku kwa mazungumzo ya kabla ya mkutano rasmi na kuongeza kuwa maswali kuhusu lengo halisi, uanachama na utekelezaji bado hayajatatuliwa.

Prag | Gipfeltreffen von 44 Ländern
Waziri mkuu wa Czech Petr Fiala na mwenzake wa Uingereza Liz Truss mjini PraguePicha: David Tanecek/CTK/dpa/picture alliance

Baadhi ya mataifa tayari yamepuuzilia mbali jumuiya hiyo ya EPC na kuitaja tu kuwa ya maneno matupu na itakayokuwa vigumu kudhibiti sio tu kwa sababu ya ukubwa wake lakini pia kutokana na tofauti kubwa zilizopo zinazojumuisha ushindani wa kawaida kati ya mataifa mengi wanachama wa jumuiya hiyo kutoka Armenia na Azerbaijan hadi Ugiriki na Uturuki. Wengine wameona matumaini kwa uamuzi wa waziri mkuu wa Uingereza Liz Truss wa kuhudhuria mkutano huo kuwa ishara ambayo huenda ikafungua njia ya ushirikiano bora kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza ambao umedhoofishwa na mvutano baada ya kujitoa kwa Uingereza katika Umoja huo almaarufu Brexit na suala la Ireland Kaskazini.

Tofauti nyingine zinazotarajiwa

Hata hivyo, mkutano huo huenda ukakumbwa na tofauti kuhusu jinsi ya kupunguza bei ya gesi ili kudhibiti gharama za nishati zinazoongezeka kutokana na vita nchini Ukraine.

Miongoni mwa mataifa hayo 27 ya Umoja wa Ulaya, mvutano pia huenda ukatokea kuhusu mfuko wa msaada wa dola bilioni 197.50 wa Ujerumani kuzisaidia biashara na familia,  ambao nchi nyingi wanachama zinaukosoa kwa kuharibu ushindani kwenye soko la pamoja la Umoja wa Ulaya.