1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Beijing.

Mtullya, Abdu Said24 Oktoba 2008

Viongozi wa nchi za Ulaya na Asia waahidi mageuzi katika mfumo wa fedha duniani.

https://p.dw.com/p/FgJ2
Kansela Angela Merkel mjini Beijing.Picha: AP

Kansela Angela Merkel  wa Ujerumani ametoa mwito juu ya kuimarisha wajibu wa shirika  la fedha la  kimataifa  IMF ,katika nyakati  hizi ngumu  ambapo dunia inakabiliwa  na  mgogoro wa fedha.

Kansela Merkel amesema  hayo leo kwenye mkutano   wa viongozi wa Ulaya na bara la Asia unaofanyika mjini Beijing kujadili  mgogoro huo.


Kansela Merkel  amesema dunia  sasa inahitaji kuwa  na utaratibu mzuri. Ameeleza kuwa hayo yana maana  ya kuimarisha wajibu wa shirika la fedha la kimataifa IMF, katika kuleta  utengemavu katika  mfumo wa  fedha  duniani.

Kiongozi huyo  wa Ujerumani anaehudhuria mkutano wa kilele  wa viongozi  wa  Ulaya  na wa nchi  za jumuiya  ya  Asem mjini  Beijing pia ametoa mwito juu  ya  kuwapo  uwazi  na taratibu imara katika kudhibiti  mosoko ya fedha  , ili kusaidia katika  juhudi za kuukabili  mgogoro wa fedha  uliopo sasa.


Viongozi hao kutoka Ulaya  na nchi  za Asia pia   wanajadili njia za kukabiliana na mgogoro wa  fedha ambao  pia umezikumba nchi  za Asia.

Akifungua  mkutano  huo leo, rais Hu Jintao wa China amesema, mgogoro  wa fedha ulioanzia nchini Marekani kutokana  na watu kushindwa kulipa mikopo ya nyumba, umeathiri uchumi wa dunia nzima.

Amesema mgogoro huo unaathiri misingi ya maisha ya watu wote. Ameeleza kuwa mgogoro  huo ni  Changamoto inayopaswa kukabiliwa na nchi zote duniani, kwa pamoja.

Akisisitiza  umuhimu  wa kushirikiana katika  kuukabili mgogoro wa fedha ulioikumba dunia, naye rais wa  tume ya Umoja  wa Ulaya Jose Manuel Barosso amezitaka  nchi kutojaribu kukwepa changamoto  inayotokana  na mgogoro uliopo kwa kujitenga na kushughulikia mambo ya ndani  kitaifa.

Amekumbusha kuwa  nchi  zote zimenufaika na   biashara  huru. Kwa hiyo lazima  nchi  zote   ziepukane na tabia  ya kujenga  kuta ili kujitenga  na wengine.

Akizungumza kwenye mkutano huo rais Nicolas   Sarkozy wa Ufaranya  ambae kwa  sasa  anauongoza Umoja  wa Ulaya amezitaka  nchi za  Asia   ziziunge mkono nchi  za Ulaya kwenye mkutano muhimu  juu ya uchumi  utakaofanyika Washington  mwezi  ujao.  ambapo viongozi kutoka nchi 20 , tajiri na zinazoinukia  kiuchumi, pia  watajadili njia za kuutatua mgogoro wa fedha.

Rais Sarkozy pia ametoa mwito wa kuleta mageuzi katika taratibu za shirika la fedha la kimataifa IMF na  katika taasisi  zingine zote zilizoundwa baada ya  kumalizika  vita kuu vya pili mwaka 1945.

Viongozi  wa  Ulaya na  wa Asia wa jumuiya ya  Asem   kwenye mkutano wa Beijing  wanatarijiwa  kuwafiki  wajibu wa shirika la IMF katika kuzisaidia nchi zilizoathirika kwa  kiwango kikubwa  na mgogoro wa  fedha.