1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa waandishi wa habari waingia siku ya pili Bonn

Charo Josephat4 Juni 2009

Miongoni mwa mada za leo ni Somalia na vyombo vipya vya habari

https://p.dw.com/p/I3DT
Wajumbe kwenye mkutano wa BonnPicha: DW

Mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari umeingia siku yake ya pili hii leo hapa mjini Bonn Ujerumani. Mkutano huo unafanyika kwa mara ya pili na kauli mbiu ya mwaka huu ni kuzuia mizozo kutumia teknolojia mpya ya mawasiliano wakati huu wa enzi ya matumizi ya aina mbalimbali za mifumo ya mawasiliano.

Hii leo wajumbe watajadili maswala mbalimbali yakiwemo vita vya kupigania masafa ya kutangazia na vipi waandishi wa habari wanavyotakiwa kujichukulia katika maeneo ya mizozo. Kutakuwa na mjadala kuhusu fedha na vyombo vya habari na athari zilizosababishwa na mgogoro wa kiuchumi.

Mijadala mingine itahusu siasa na vyombo vya habari na mizozo inayojitokeza baada ya uchaguzi na umuhimu wa mtandao wa kijamii wa "twitter" kama chombo muhimu kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari. Somalia itajadiliwa kwa mtizamo wa vyombo vipya vya habari na vipi jamii ya Wasomali wanaoishi nje ya nchi wanavyoweza kuingilia kati katika kutatua mzozo nchini mwao.

Akizungumza kwenye mkutano huo hapo jana, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Soon – Hong Choi, alisema kuainisha na kuwa na njia moja ya kukusanya habari kabla na wakati wa mizozo kunaweza kusaidia kupitisha maamuzi na utoaji wa huduma kwa wakati muafaka kwa wale wanaohitaji msaada.

Kiongozi huyo aidha amesema upatikanaji wa habari za uhakika, za kutegemewa, zilizo kamili na ambazo hazijapitwa na wakati, kunaweza pia kuchangia katika kuboresha upashaji wa habari kwa umma na uandishi wa habari kwa jumla.

Soon-Hong Choi amesema mkutano wa waandishi wa habari mjini Bonn ni wa umuhimu mkubwa na kulipongeza shirika la habari la Deutsche Welle kwa kuandaa mkutano huo.

"Ulimwengu wa habari uko katika mabadiliko. Bila shaka mabadiliko haya yataathiri hali ya baadaye ya vyombo vya habari, uandishi na utangazaji wa habari na usimamizi. Kwa mantiki hii, ningependa kuishukuru Deutsche Welle kwa kuandaa jukwaa hili la waandishi wa habari kujadili swali hili linalojitokeza."

Global Media Forum Teilnehmer Erik Bettermann
Mkurugenzi mtendaji wa Deutsche Welle Erik BettermannPicha: DW

Akihutubia kikao cha jana bwana Gunter Nooke, mjumbe wa haki za binadamu wa serikali ya Ujerumani amesema ni vyema kwamba wakati huu hakuna kiongozi yeyote wa kiimla duniani anayeweza kufanya atakalo bila kugonga vichwa vya habari. Inatia moyo pia kwamba tunaweza kupata habari kuhusu mateso yanayowakabili raia wasio na hatia katika maeneo ya mizozo kama nchini Sri Lanka na Pakistan.

Lakini swali linalojitokeza ni jambo gani linaposwa kufanywa baada ya kupata habari hizo. Kwa mtazamo wake anasema,"Kwamba tujadiliane kwa uaminifu ili matakwa yetu na uaminifu wetu visitengane. Kwa misingi hii hatuwezi kufumbia macho wala kukubali ukiukaji wa haki za binadamu ulimwenguni kote."

Mkutano huo wa kimataifa wa waandishi wa habari utamalizika hapo kesho.

Mwandishi: Josephat Charo/www.dw-gmf.de

Mhariri: Saumu Mwasimba