1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa Jeshi la Misri astaafishwa

13 Agosti 2012

Rais wa Misri Mohammed Morsi amemuamuru waziri wa ulinzi Field Marshal Hussein Tantawi kustaafu. Uamuzi wake umechukuliwa kama hatua ya kuimarisha mamlaka yake na kudhibiti ushawishi wa jeshi.

https://p.dw.com/p/15oZC
Field Marshal Hussein Tantawi
Field Marshal Hussein TantawiPicha: dapd

Uamuzi wa Rais Mohammed Morsi kumstaafisha ghafla Field Marshal Hussein Tantawi kutoka wadhifa wa waziri wa Ulinzi umetangazwa na msemaji wake Yasser Ali, ambaye pia amesema rais huyo amelibatilisha agizo la kikatiba linalolipa jeshi madaraka makubwa ya na kauli juu ya sheria zinazotungwa nchini humo. Tangazo hilo limeashiria sura mpya katika uhusiano baina ya Mohammed Morsi ambaye ni rais wa kwanza wa kiraia kuiongoza Misri, na jeshi ambalo jeshi ambalo limekuwa likitaka kuyawekea kikomo mamlaka yake.

Jenerali Abdel Fattah al-Sisi ambaye alikuwa katika kitengo cha upelelezi ameteuliwa kuchukua na fasi ya Field Marshal Tantawi. Akizungumza kwenye muskiti wa Al-Azhar mjini Cairo baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo, rais Morsi alisema uamuzi huo umechukuliwa kwa maslahi ya taifa.

''Uamuzi ambao nimeupitisha haukumlenga mtu yeyote binafsi, na sikudhamiria kwa hali yoyote kuiadhiri taasisi yoyote ile. Mungu ni shahidi wangu, uamuzi huo nimeuchukua kwa maslahi ya taifa na ya watu wa nchi hii.'' Alisema Morsi.

Nafasi kwa kizazi kipya

Rais Mohammed Morsi amesema uamuzi wake ulikuwa kwa maslahi ya taifa
Rais Mohammed Morsi amesema uamuzi wake ulikuwa kwa maslahi ya taifaPicha: picture-alliance/dpa

Aidha, Rais Morsi amesema hatua aliyochukua inalenga kuupa dira mustakabali wa Misri, na kutoa nafasi kwa kizazi kipya. Maelfu ya watu wanaomuunga mkono, hususan wale kutoka kikundi cha Udugu wa Kiislamu, walikusanyika kwenye uwanja wa Tahrir kusherehekea uamuzi wa kumstaafisha Hussein Tantawi, ambaye alishikilia hatamu za uongozi wa Misri kwa kipindi cha mwaka mmoja kufuatia kuangushwa kwa utawala wa rais Hosni Mubarak.

Watu hao walipaza sauti wakisema wanamuunga mkono rais, na kutoa ishara za dhihaka kwa Field Marshal Hussein Tantawi.

Msemaji wa rais Morsi amesema kuwa Hussein Tantawi na kamanda mkuu wa jeshi la Misri Sammi Anan ambaye pia ameamliwa kung'atuka, wamepewa tuzo ya juu kabisa nchini humo, na kuendelea kuwa washauri wa rais.

Uamuzi sahihi kwa wakati muafaka

Afisa mmoja wa ngazi za juu katika chama cha Uhuru na haki chenye mafungamanao na kikundi cha Udugu wa Kiislamu, Mourad Ali, amesema uamuzi wa rais Morsi umechukuliwa kwa wakati muafaka. Vyanzo kutoka ndani ya jeshi la Misri ambavyo havikutajwa majina vimenukuliwa na shirika la habari la Misri MENA, wakisema rais Morsi alijadiliana na maafisa wakuu jeshini kabla ya kuchukua uamuzi wa kumstaafisha Hussein Tantawi.

Field Marshal Tantawi aliongoza Baraza la Kijeshi lililotawala katika kipindi cha mpito
Field Marshal Tantawi aliongoza Baraza la Kijeshi lililotawala katika kipindi cha mpitoPicha: picture alliance / dpa

Wiki iliyopita, mkuu wa upelelezi wa Misri Muraf Muwafi pia alipewa amri ya kustaafu, baada ya mashambulizi kwenye rasi ya Sinai, ambamo wanajeshi 16 wa Misri waliuawa na wanamgambo. Wakati hayo yakiiarifiwa, wanamgambo hao hao wamemuua leo chifu wa kijadi katika eneo la Sinai, wakati jeshi likiwa linaendelea na operesheni dhidi yao, ambayo ni kubwa kabisa tangu kukabidhiwa eneo hilo kutoka Israel mwaka 1973.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE

Mhariri:Josephat Charo