1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa yuko Syria

7 Machi 2012

Syria imesema iko tayari kushirikiana na ujumbe wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa unaozuru nchini humo ili kutafuta ruhusa ya kuingia katika miji inayokumbwa na mashambulio.

https://p.dw.com/p/14GdU
UN-Nothilfebeauftragte Valerie Amos mit dem syrischen Außenminister Walid al-Moualem In this photo released by the Syrian official news agency SANA, U.N. humanitarian chief Valerie Amos, left, meets with Syrian Foreign Minister Walid al-Moallem at the Syrian foreign ministry, in Damascus, Syria, Wednesday, March 7, 2012. The U.N. humanitarian chief headed to the shattered central Syrian city of Homs on Wednesday, where activists have accused regime forces of trying to cover up evidence of a monthlong military assault and alleged execution-style killings. (Foto:SANA/AP/dapd)
UN-Nothilfebeauftragte Valerie Amos in Damaskus OVERLAYPicha: SANA

Shirika la habari la serikali SANA limesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Syria Walid al-Mualem baada ya mkutano na Mkuu wa Masuala ya Kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa Valarie Amos, alisisitiza dhamira ya Syria kushirikiana na ujumbe huo kwa misingi ya heshima, himaya na uhuru wa Syria na kwa ushirikiano na Wizara ya mambo ya kigeni.

Awali msemaji wa ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA aliliambia shirika la habari la Reuters mjini Geneva kuwa Bibi Amos tayari amemaliza mkutano na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria.

Maafisa wazuiwa kuingia maeneo ya machafuko

Amos ambaye alinyimwa kibali cha kuingia Syria wiki iliyopita, aliwasili nchini humo akiwa katika ujumbe wa ziara ya siku tatu ya kujaribu kuushawishi utawala kuwaruhusu wafanyakazi wa misaada ya dharura kuingia ndani ya maeneo ya machafuko na kuwapa raia usaidizi wa kuokoa maisha.

Hali ya kibinadamu imezidi kwua mbaya Syria
Hali ya kibinadamu imezidi kwua mbaya SyriaPicha: AP

Shirika hilo la ulimwengu limezuiwa nchini Syria ambako Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC ndilo shirika la pekee linalokubaliwa kuwatuma wafanyakazi wake nchini humo na kusambaza chakula na vifaa vya matibabu.

Lakini mamlaka ya Syria yameendelea kulizuia shirika la ICRC kuingia katika wilaya ya Baba Amr ya mkoa unaokabiliwa na mashambulio Homs, ambako Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti za vikosi vya serikali vimewauwa, kuwazuia na kuwatesa watu.

Msafara wa shirika la Msalaba Mwekundu umekuwa ukisubiri kuingia Baba Amr tangu Ijumaa iliyopita, siku moja baada ya wapiganaji waasi kuondoka eneo hilo kufuatia mwezi mmoja wa mashambulio ya vikosi vya serikali.

Mashambulio yaendelea Syria

Nchini Syria kwenyewe, Baraza la Taifa la Syria ambalo ni kundi kuu la upinzani limesema vifaru na magari ya kijeshi yalionekana yakielekea katika wilaya ya Baba Amr katika mkoa wa Kaskazini Magharibi Homs.

Mashambulio ya vikosi vya serikali yaendelea Homs
Mashambulio ya vikosi vya serikali yaendelea HomsPicha: picture-alliance/dpa

Taarifa ya baraza hilo imesema kumeonekana vifaru 42, na magari 131 ya kijeshi yakiondoka Latakia kuelekea mji wa Saraqb mkoani Idlib, huku msafara mwingine wa kijeshi ukiondoka mkoa huo wa Idlib.

Baraza hilo limeongeza kuwa wapiganaji kadhaa waliuwawa katika mashambulio ya Maaret al-Numan ambao ni mji mwingine wa mkoa wa Idlib.

Wakati huo huo Shirika la Safari za Ndege la Ufaransa limesema leo kuwa linasitisha safari zake zote za kwenda mjini Damascus kutokana na hali inayozidi kuzorota nchini Syria. Msemaji wa Shirika la Air France-KLM amesema hatua hiyo imechukuliwa hadi wakati usiojulikana. Shirika hilo lina safari tatu kwa wiki hadi Damascus kupitia Amman kila Jumatatu, Alhamisi na Jumamosi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri:Josephat Charo