1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa polisi Uganda azusha hasira

1 Februari 2016

Makundi ya upinzani Uganda yakasirishwa na kauli za mkuu wa polisi ya taifa aliyenukuliwa katika gazeti moja akikiambia kikosi cha kiraia kinachopambana na uhalifu kujiandaa kwa “vita” baada ya uchaguzi wa rais

https://p.dw.com/p/1Hl5N
Uganda Polizei in Kampala
Picha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Polisi ilikanusha kuwa kamanda huyo mkuu alitoa kauli hiyo. Rais Yoweri Museveni, mpiganaji wa zamani wa vita vya msituni ambaye ameiongoza Uganda tangu mwaka wa 1986, anakabiliwa na ushindani mkali kabla ya uchaguzi wa Februari 18, ambapo atapambana na aliyekuwa waziri mkuu wake, Amama Mbambazi na kiongozi wa upinzani wa muda mrefu Kizza Besigye.

Katika mkutano na “wazuia uhalifu”, kikosi cha kujitolea kinachoundwa na kusimamiwa na polisi na ambacho wanachama wake wanatuhumiwa kwa kufanya mashambulizi dhidi ya wakosoaji wa serikali, mkuu wa polisi Kale Kayihura alisema kundi hilo linapaswa kuweka ulinzi kuzuia wizi wa kura utakaofanywa na upinzani.

Afrika Uganda Protest Amama Mbabazi ehem. Premierminister Polizei Jinja
Polisi wakipambana na wafuasi wa Amama MbabaziPicha: Reuters/James Akena

Kwa mujibu wa gazeti la The Observer, Kayihura aliliambia kundi hilo la wazuia uhalifu na namnukuu “hatutakabidhi madaraka kwa upinzani ili kuvuruga amani ambayo tulipigania”. Aliendelea kusema “katiba inawapa polisi mamlaka ya kuilinda nchi ikiwa kuna vita na nataka mjiandae kwa hilo”.

Msemaji wa polisi Fred Enanga aliliambia shirika la Reuters kuwa habari ya gazeti hilo “iligeuzwa kwa lengo la kujiongezea umaarufu na kuzusha utata” na akakanusha kuwa Kayihura alitoa kauli hizo. Akol Mande Amazima, mchambuzi wa kisiasa mjini Kampala anasema iwe ni kuwa matamshi hayo ni ya kweli au la, yanazusha hali ya wasiwasi kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi

Makundi ya haki za binaadamu kwa muda mrefu yameishutumu serikali ya Museveni kwa kutumia mbinu za ukamataji kinyume cha sheria unaofanywa na maafisa wa usalama ili kuwakandamiza wafuasi wa upinzani, wakati waangalizi wakisema aliiba kura katika chaguzi zilizopita. Serikali inakanusha madai ya aina hiyo. Mapema mwezi huu, Shirika la haki za binadaamu la Human Rights Watch liliitaka Uganda kuufuta mpango huo wa kuzuia uhalifu kwa kulitumia jeshi la umma. Akol anasema mpango huo mara nyingi unatumiwa vibaya na wanasiasa

Amama Mbabazi, aliiambia Reuters kuwa kundi hilo la wazuia uhalifu ni wapiganaji wa chama tawala cha NRM wanaojifanya kuwa wao ni polisi

Mchambuzi mwingine wa kisiasa Nicholas Ssengoba anasema Museveni anamtumia mkuu wa polisi kutuma ujumbe kuwa ikiwa atashindwa basi kutakuwa na madhara makubwa.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri:Iddi Ssessanga