1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa walinda amani wa UN akutana na Rais Joseph Kabila

Florence Majani18 Desemba 2017

Siku chache baada ya walinda amani 14 kutoka Tanzania kuuawa na watu wanaoshukiwa kuwa waasi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mkuu wa walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa amekutana na Rais Joseph Kabila

https://p.dw.com/p/2pZ7I
Kongo Friedenswächter ermordet
Walinzi wa amani wa UN, wakilinda katika eneo la Goma, DRC. Waasi walishambulia walinda amani na kuwaua 14 mnamo Desemba 7. Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Jean Pierre Lacroix  alifanya mazungumzo na Rais Kabila jana, ambapo waliangazia usalama na uchaguzi mpya nchini humo.Awali, Lacroix alitembelea mji wa Goma siku ya Ijumaa, na kuwaangalia walinda amani 30 waliojeruhiwa katika shambulio lililotokea katika mji wa Kivu Kaskazini, mnamo Desemba 7 mwaka huu.

Chanzo kimoja cha habari kilicho karibu na majeshi ya kulinda amani nchini Congo, MONUSCO, kimeliambia shirika la habari la AFP kuwa Kabila na Lacroix  walijadili kuhusu shambulio hilo, ambalo ni baya kabisa katika historia ya karibuni ya majeshi hayo.

Lacroix alisema machafuko katika upande wa mashariki wa Congo ni mrundikano wa matatizo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa pamoja. "Ushirikiano na nchi jirani ni muhimu sana," amenukuliwa Lacroix akizungumza kwenye Redio ya Umoja wa Mataifa.

Eneo kubwa la mashariki mwa Congo, limekabiliwa na machafuko kwa muda mrefu, lakini mapigano baina ya majeshi ya serikali na makundi ya wanamgambo, pamoja na mapambano ya kikabila yameongezeka zaidi mwaka huu.

Jimbo la Kivu Kaskazini, ambalo lipo mpakani mwa Uganda na Rwanda, limekabiliwa na mauaji  kwa kiasi kikubwa na utekaji nyara baina ya makundi ya waasi na ya kikabila.

Jean-Pierre Lacroix UN Untergeneralsekretär für Friedensmissionen
Mkuu wa Walinda amani wa Umoja wa Mataifa, Jean Pierre Lacroix. Ametembelea majeruhi walioshambuliwa katika tukio la Desemba 7 na kutoa heshima za mwisho kwa walinda amani 14 wa Tanzania waliofariki katika tukio hilo.Picha: picture-alliance/dpa
DR Kongo Kinshasa Präsident Kabila
Rais Joseph Kabila wa DRC.Picha: Imago/Xinhua

Tangu Oktoba mwaka 2014, kundi la waasi la ADF linashutumiwa na serikali mjini  Kinshasa pamoja na Umoja wa Mataifa kwa kuua watu zaidi ya 700 katika mji wa Beni, ambako shambulizi jingine limefanyika wiki iliyopita.

Nchi hiyo pia inakabiliwa na machafuko kutokana na Rais Kabila kugoma kutoka madarakani baada ya muhula wake wa mwisho kufika mnamo Desemba mwaka jana, huku akiusogeza mbele uchaguzi hadi Desemba 2018.

Lacroix amesema, mchakato huo ni wajibu wa viongozi wa Congo. Alisema UN imeonyesha dhamira ya kushiriki katika mchakato huo.Siku moja baada ya shambulio hilo, Lacroix alinukuliwa na shirika la habari la AP akisisitiza kuwa lengo la walinda amani hao ni kulinda raia.

Awali akiwa katika hospitali ya Goma, Lacroix aliwaambia walinda amani waliojeruhiwa katika shambulio la Desemba 7 kuwa amekwenda Tanzania pia  na kwamba kwamba nchi hiyo ipo pamoja nao.

Lacroix alikuwa jijini Dar es Salaam Alhamis ya wiki iliyopita na kutoa heshima zake za mwisho kwa walinda amani 14 wa Tanzania waliouawa katika tukio hilo. Walinda amani watano wa Congo waliuawa pia katika shambulio hilo, lililowajeruhi wengine 53.

Mwandishi: Florence Majani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef