1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 29 wajeruhiwa katika mlipuko wa bomu Cairo

20 Agosti 2015

Kundi la Dola la Kiislamu tawi la Misri limesema ndilo lililohusika na mlipuko wa bomu la kutegwa ndani ya gari lililowajeruhi watu 29 karibu na jengo la usalama wa taifa na mahakama mapema leo (20.08.2015)

https://p.dw.com/p/1GIDM
Ägypten Bombenanschlag in Kairo
Picha: Reuters/M.A. El Ghany

Taarifa iliyosambazwa kwenye mtandao wa Twitter na wafuasi wa kundi hilo, la Mkoa wa Sinai, imesema kuwa bomu hilo lilikuwa la kulipiza kisasi mauaji ya wanachama wake sita waliohukumiwa kwa kufanya shambulizi kaskazini mwa mji huo mkuu wa Misri mwishoni mwa mwaka jana.

Mnamo mwezi Mei, Misri iliwanyonga wanachama sita wa Mkoa wa Sinai, tawi la kundi la Dola la Kiislamu nchini Misri kwa kuwashambulia wanajeshi mwaka wa 2014 ambapo wanajeshi wawili waliuawa katika kijiji cha Araba Sharkas kaskazini mwa Cairo.

Wanamgambo wa Mkoa wa Sinai wamewauwa mamia ya wanajeshi na polisi tangu jeshi lilipomwondoa madarakani Mohamed Mursi wa Kundi la Udugu wa Kiislamu mwaka wa 2013 baada ya maandamano ya umma dhidi ya utawala wake.

Ägypten Sinai Sicherheit Polizei Terror
Misri inapambana na wanamgambo katika Rasi ya SinaiPicha: picture-alliance/dpa/Gharnousi/Alyoum

Duru za usalama zilizokagua eneo la mlipuko wa asubuhi la Shubra al-Khaima karibu na Cairo zimesema kulikuwa na gari lililochomeka na shimo kubwa barabarani. Wanamgambo wenye makao yake katika Rasi ya Sinai ambao wanaunga mkono Dola la Kiislamu, ambalo linayadhibiti maeneo ya Iraq na Syria na pia wana uwepo katika nchi jirani Libya, wanastahimili operesheni zinazofanywa na jeshi.

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi ameapa kuangamiza uasi, ambao anasema ni kitisho kikubwa kwa ulimwengu wa Kiarabu na mataifa ya Magharibi.

Juhudi za kuimarisha usalama zaendelea

Kurejesha utulivu nchini Misri ni muhimu kwa juhudi za kuujenga upya uchumi ulioharibiwa na machafuko tangu vuguvugu la umma la mwaka wa 2011 ambalo lilimwangusha aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Hosni Mubarak

Mamlaka za Misri zinaendesha operesheni kali ya usalama dhidi ya wanamgambo kuwahi kufanywa katika historia ya nchi hiyo, hali inayozusha shutuma kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binaadamu ambayo yanaituhumu serikali kwa kuunyamazisha upinzani.

Mwezi huu, Rais Sisi aliidhinisha sheria ya kupambana na ugaidi ambayo inatoa nafasi ya kuundwa mahakama maluum katika wakati ambapo uasi wa miaka miwili unaofanywa na makundi ya itikadi kali unalenga kuiangusha serikali yake.

Sheria hiyo imekosolewa vikali na makundi ya haki za binaadamu ambayo yanamshtumu Sisi kwa kuuangamiza uhuru uliopatikana baada ya wimbi la mageuzi la mwaka wa 2011.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga