1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mmiliki wa Wikileaks afikishwa mahakamani

7 Desemba 2010

Julian Assange amefikishwa katika mahakama moja mjini London, baada ya kukamatwa na polisi kwa tuhuma za ubakaji zinazomkabili.

https://p.dw.com/p/QRi0
Mmiliki wa mtandao wa Wikileaks, Julian Assange.Picha: Picture alliance/dpa

Mwanzilishi wa mtandao wa WikiLeaks, Julian Assange, amefikishwa katika mahakama moja mjini London, Uingereza kujibu mashtaka ya ubakaji yanayomkabili, baada ya kamatwa na polisi mjini London hii leo kutokana na waranti wa kukamatwa kwake uliotolewa na Sweden akihusishwa na tuhuma hizo.

Julian Assange raia wa Australia na ambaye mtandao wake wa Wikileaks umekosolewa vikali kutokana na kuchapisha nyaraka za siri za kidiplomasia za Marekani, amekamatwa kulingana na waranti wa Umoja wa Ulaya. Assange, mwenye umri wa miaka 39 alikamatwa baada ya kujisalimisha mwenyewe kwa makachero katika kituo cha polisi cha London. Kesi yake inabidi kusikilizwa ndani ya siku 21, baada ya kukamatwa kwake.

Waendesha mashtaka wa Sweden wanataka kumhoji Assange kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo ya ubakaji. Hata hivyo, amezikanusha tuhuma hizo dhidi yake. Mtandao wa Wikileaks ambao ulisababisha hasira na ghadhabu nchini Marekani kutokana na kuchapisha nyaraka hizo, umeahidi kuendelea kuchapisha hadharani nyaraka 250,000 za siri ambazo inazo kuhusu Marekani. Taarifa iliyotolewa na Wikileaks kupitia mtandao wa mawasiliano ya kijamii ya Twitter, imeeleza kuwa kukamatwa kwa Assange hakutazuia kutolewa kwa nyaraka hizo na kuathiri shughuli zake.

Assange ametumia muda wake mwingi nchini Sweden na mwanzoni mwa mwaka huu alituhumiwa kwa kuhusika na uhalifu wa ngono alioufanya dhidi ya wanawake wawili raia wa Sweden, ambao walikuwa wanafanya kazi kwa kujitolea katika mtandao wa Wikileaks. Novemba 18 mwaka huu mahakama moja mjini Stockholm, Sweden ilitoa waranti wa kukamatwa kwa Assange kwa ajili ya kuhojiwa, kuhusiana na tuhuma za ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia na matumizi ya nguvu kinyume cha sheria.

Tuhuma hizo ziliwasababisha waendesha mashitaka wa Sweden kumfungulia mashtaka na kisha kuyafutilia mbali kabla ya kuyafungua tena na uchunguzi dhidi ya mashtaka hayo kuendelea. Mashtaka yanayomkabili Assange huenda yakasababisha kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela iwapo atapatikana na hatia.

Polisi wa London wamesema kuwa Assange alikamatwa majira ya saa tatu na nusu asubuhi na polisi wa kitengo kinachohusika na kuwarudisha washukiwa katika nchi zao husika, baada ya kufika kituoni hapo kwa miadi. Hata hivyo, mahali alipokuwa akiishi Assange hapajulikani. Mawakili wa Assange hawakupatikana mara moja kuzungumzia hatua ya kukamatwa kwa mteja wao, lakini wamesema kuwa watapinga mteja wao kurejeshwa Sweden kwa kuwa wana hofu huenda akahamishiwa Marekani.

Mmoja wa mawakili wake aliyeko London, Jennifer Robinson, amesema kuwa mteja wake alitengwa na kuteswa na kwamba vitisho vya kifo vimekuwa vikitolewa katika blogu mbalimbali dhidi ya mtoto wa kiume wa Assange. Wikileaks tayari imefukuzwa nchini Marekani ambako wanasiasa wametaka mmiliki wake achukuliwe kama gaidi. Maafisa wa Uswisi jana wamefunga akaunti za benki za Assange, huku mfadhili mkubwa wa Wikileaks akiwa matatani nchini Ujerumani kwa kushindwa kujaza akaunti zake kwa muda unaotakiwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman