1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mmoja auawa Munich katika shambulio la kisu

Admin.WagnerD10 Mei 2016

Mtu mmoja ameuwawa na wengine watatu wamejeruhiwa katika shambulio la kisu katika kituo cha treni mashariki mwa mji wa Munich mapema leo Jumanne(10.05.2016), na kwamba tukio hilo huenda lina hamasa za kisiasa.

https://p.dw.com/p/1Ikyd
Deutschland Polizist in Herborn stirbt nach Messerattacke
Polisi wakifunga kituo cha treni cha GrafingPicha: picture-alliance/dpa/F. Rumpenhorst

Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 50 amefariki kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kupelekwa hospitali, waendesha mashitaka na ofisi ya uchunguzi wa makosa ya jinai katika jimbo la Bavaria nchini Ujerumani limesema.

Wachunguzi wamesema mshambuliaji aliwarukia ghafla mtu huyo pamoja na wahanga wengine watatu wakiwa na umri kati ya miaka 43 na 58 katika kituo cha treni katika mji wa Grafing, mji ulioko kilometa 30 mashariki mwa Munich. Wameongeza kwamba mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 27 ni raia wa Ujerumani.

Deutschland Messerattacke am Grafinger Bahnhof
Kituo cha treni kulipotokea shambulio la kuchomwa kisu watu wannePicha: Reuters/M. Rehle

Polisi imesema mshukiwa alikamatwa katika eneo la tukio na uchunguzi wa kihalifu umeanzishwa na maafisa katika jimbo la kusini la Bavaria.Msemaji wa polisi ya Bavaria Hans-Peter Kammerer amesema mshambuliaji alitamka maneno yenye hamasa za kisiasa.

Hamasa za kisiasa

"Hatuwezi bado kujua sababu za shambulio hilo. Ni Mjerumani mwenye umri wa miaka 27. Alikuwa na kisu na wakati wa shambulio alitoa matamshi mbayo yanaweza kuelezewa kuwa yana hamasa za kisiasa. Hatuwezi kuondoa uwezekano wa hamasa za kisiasa katika shambulio hili."

Redio ya mjini Bayern , Bayerischer Rundfunk imeripoti kwamba mshambuliaji alipiga keleke akisema "Allahu Akbar," ama "Mungu ni mkubwa," kwa mujibu wa watu walioshuhudia katika eneo la tukio.

Kituo hicho cha treni kilifungwa baada ya mtu huyo kukamatwa.

"Hakuna tena kitisho kwa umma," amesema msemaji wa polisi , Michaela Gross.

Deutschland Messerattacke am Grafinger Bahnhof
Kituo cha treni cha Grafing karibu na MunichPicha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Mwezi Agosti mwaka jana, wapiganaji wawili wa jihadi ambao wanahusika katika kundi la Dola la Kiislamu walitishia kuishambulia Ujerumani katika vidio iliyowekwa katika mtandao wa intaneti.

Katika vidio hiyo iliyotolewa kwa lugha ya Kijerumani wamewataka wale waliowaita "kaka na dada zao" nchini Ujerumani na Austria kufanya mashambulizi dhidi ya kile waliochoeleza kuwa ni "wasio amini" hapa nyumbani.

Mashambulio ya visu

Tangu wakati huo Ujerumani imeshuhudia kiasi mashambulio mawili ya visu ambayo yanahusishwa na Waislamu wenye itikadi kali, kabla ya shambulio la leo.

Mwezi Februari msichana mwenye umri wa miaka 15 aliyetambulika kama Safia S. alimchoma kisu polisi shingoni katika kile waendesha mashitaka baadaye walichosema ni shambulio lenye ushawishi wa mashambulio ya IS.

Deutschland Messerattacke am Grafinger Bahnhof
Mtu mmoja ameuwawa baada ya kuchoma kisu katika kituo cha treni cha GrafingPicha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Waendesha mashitaka wa shirikisho baadaye wamesema msichana huyo, alikuwa anakumbatia nadharia za itikadi kali za jihadi za kundi la kigeni la magaidi la Dola la Kiislamu lililoko nchini Iraq na Syria, na amekuwa na mahusiano na wapiganaji wa IS nchini Syria.

Septemba mwaka jana mtu mmoja kutoka Iraq mwenye umri wa miaka 41 aliyetambuliwa kama Rafik Y. alimchoma kisu na kumjeruhi vibaya polisi mwanamke mjini Berlin kabla ya afisa mwingine kupigwa risasi na kufa.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef