1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

​​​​​​​Mo Farah asisitiza yeye mwanariadha safi

Isaac Gamba
27 Februari 2017

Bingwa mara nne wa riadha wa Olimpiki Mo Farah amesisitiza kwa mara nyingine tena kuwa ni mwanariadha aliye na rekodi bora

https://p.dw.com/p/2YJfY
Olympia Rio 16 20 08 Momente 5000 Meter Herren Mo Farah
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Mwanariadha huyo muingereza anayengara katika mbio za masafa ya kati alikanusha madai hayo hapo jana na kusema kuwa hajawahi kutumia madawa kwa ajili ya kusisimua misuri na kuwa taarifa hizo zilizoibuliwa na vyombo vya habari zinamuweka katika mazingira mabaya kimchezo licha ya kuwa amekuwa akizikanusha mara kwa mara.

Farah aliye na umri wa miaka 33 kwa sasa amekanusha taarifa hizo baada ya gazeti la Sunday Times kuchapisha habari likimhusisha kocha wake Alberto Salazar na matumizi ya madawa hayo kwa wanariadha wake. Gazeti la Times linadai kuwa taarifa yake kuhusiana na suala hilo linatokana na taarifa zilizovuja mnamo Machi 2016 kutoka shirika la kupambana dhidi ya madawa ya kuongeza nguvu michezoni (USADA). Shirika hilo linaendelea na uchunguzi wake dhidi ya kocha huyo wa Mo Farah kuhusiana na matumizi ya madawa hayo kwa wachezaji wake.

Mo Farah ambaye alijizolea medali baada ya kushinda mbio za mita 5,000 na mita 10,000 mnamo mwaka 2012 na 2016 amesema iwapo USADA ama taasisi nyingine yoyote ina ushahidi dhidi yake wa kutumia madawa hayo basi wauchapishe hadharani ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua badala ya kuviachia vyombo vya habari kuhukumu.

Mwandishi: Isaac Gamba
Mhariri: Yusuf Saumu