1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Modi aahidi India mpya

16 Mei 2014

Waziri Mkuu mteule wa India, Narendra Modi, ameahidi kutimiza ndoto za raia bilioni 1.2, huku chama tawala cha Congress kikiri kushindwa na viongozi kadhaa wa kimataifa wakimpongeza Modi kwa ushindi wa kishindo.

https://p.dw.com/p/1C1Qb
Waziri Mkuu mteule wa India, Narendra Modi.
Waziri Mkuu mteule wa India, Narendra Modi.Picha: Reuters

Maelfu ya wafuasi wa Modi wamemiminika kwenye jimbo la Vadodara, Gujarat, mchana wa leo, kumsikiliza kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 63 akihutubia umma kwa mara ya kwanza tangu kukipatia chama chake cha wazalendo wa Kihindu ushindi mkubwa.

Modi amewaambia wafuasi hao kwamba sasa joto la uchaguzi limekwisha na kwamba watu wametoa uamuzi wao wa kuitaka India isonge mbele kutimiza ndoto za roho bilioni moja na milioni mia mbili za raia wa nchi hiyo. Ameahidi kufanya kazi na wapinzani wake kwa manufaa mapana ya taifa.

Kabla ya mkutano huo, kiongozi wa chama cha Congress, Sonia Gandhi, alifanya mkutano na waandishi wa habari, ambapo alitangaza rasmi kushindwa kwa chama chake na kumtakia kheri Modi na BJP.

"Uamuzi huu kwa hakika uko dhidi yetu, lakini tunauheshimu uamuzi wa watu kwa moyo wote. Hata hivyo, tunatazamia kwamba serikali mpya ya shirikisho haitakuwa na uvumilivu dhidi ya wanaochafua umoja wa kijamii na maslahi ya nchi."

Mtoto wa Gandhi, Rahul, ambaye aliongoza kampeni ya chama hicho cha Congress, kinachochukuliwa kama chama cha familia yake, alisema yeye binafsi ndiye wa kulaumiwa kwa kushindwa huko, na kwamba ana kazi kubwa ya kufanya kurekebisha makosa yaliyowanyima ushindi.

Ushindi wa aina yake

BJP imejizolea zaidi ya viti 272 vya bunge, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1984 kwa chama kimoja tu kuzoa viti vinavyotosha kuunda serikali peke yake.

Wafuasi wa Modi wakishangiria ushindi wa chama chao cha BJP.
Wafuasi wa Modi wakishangiria ushindi wa chama chao cha BJP.Picha: UNI

Hata hivyo, wakosoaji wake wanaonya kwamba kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 63 anaweza kukabiliwa na mgogoro wa kidini, kwani chama chake chenye misingi ya uzalendo wa Kihindu kimewahi kutuhumiwa kuwa dhidi ya jamii ya Waislamu milioni 150 raia wa nchi hiyo.

Mnamo mwezi Januari, Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Manmohan Singh alionya kwamba Modi atakuwa janga kwa nchi.

Mwaka 2002, mataifa ya magharibi yalimuwekea vikwazo vya kusafiri Modi kwa sababu ya ushiriki wake kwenye ghasia za kidini zilizoua watu wapatao 1,000 kwenye jimbo la Gujarat, ambalo yeye alikuwa waziri kiongozi.

Uingereza, Pakistan zampongeza Modi

Katika hatua nyengine, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amemualika rasmi Modi kuitembelea Uingereza, ikiwa ni ishara ya mkoloni huyo wa zamani kubadilisha sera zake juu ya waziri mkuu huyo mpya. Cameron alimpigia simu Modi asubuhi ya leo kumpongeza.

Modi akiwa na mama yake kuomba baraka kabla ya kupiga kura.
Modi akiwa na mama yake kuomba baraka kabla ya kupiga kura.Picha: Reuters

Kama zilivyokuwa nchi nyengine za Ulaya, Uingereza iliondoa marufuku yake dhidi ya Modi mwaka 2012.

Salamu kama hizo za kheri zimetoka kwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif, ambaye alimpigia simu Modi na kuuita ushindi wake kuwa ni ishara njema kwa mataifa hayo mawili.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman