1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mogadishu. Jeshi lafunga kituo kimoja cha radio.

19 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBOX

Matangazo ya kituo kimoja maarufu cha radio nchini Somalia yamekatizwa leo Jumatano baada ya wanajeshi wawili wa serikali kutishia kulishambulia jengo la radio hiyo kwa risasi na makombora.

Mkurugenzi wa radio Shabele amesema kuwa radio hiyo ilifungwa siku moja baada ya polisi ambao walikuwa wanawasaka wapiganaji kufyatua risasi nje ya jengo la kituo hicho, na kumuua mtu mmoja na wafanyakazi wa radio hiyo kukimbilia nje.

Jafar Kukay mkurugenzi wa kituo hicho , amesema baada ya shambulio hilo, kuwa wanajeshi wawili walitishia kulishambulia jengo hilo iwapo radio hiyo itaendelea na matangazo. Waziri wa habari Madobe Nunow Mohammed amesema hana habari juu ya kufungwa kwa kituo hicho. Kamati ya ulinzi wa waandishi wa habari yenye makao yake makuu mjini New York imeshutumu shambulio hilo.Waandishi wa habari nchini Somalia wamekuwa lengo la mashambulizi na waandishi 30 wamekimbia kutoka mji mkuu wa nchi hiyo mwaka huu.