1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Maafisa wa Umoja wa Afrika wako Somalia

15 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCab

Maafisa wa Umoja wa Afrika wamewasili nchini Somalia kukamilisha mipango ya uwekaji wa vikosi vya kulinda amani nchini humo.

Serikali ya mpito ya Somalia imeomba wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika kuwekwa nchini humo baada ya wanajeshi wake wakisaidiwa na wale wa Ethiopia kuwan’gowa wanamgambo wa Kiislam katika shambulio la mwezi wa Desemba mwaka jana.

Wakati huo huo wanajeshi wa serikali hapo jana wameanza msako wa silaha katika mji mkuu wa Mogadishu katika jitihada mpya za kurudisha utulivu mjini humo kufuatia vita viliyvodumu kwa wiki kadhaa.Msako huo unakuja siku moja baada ya bunge la Somalia kutangaza hali ya hatari ya miezi mitatu nchini humo.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika wiki hii lilikubali kuongeza idadi ya wanajeshi kutoka kikosi cha wanajeshi 8,000 kilichopendekezwa kuwekwa Somalia na imeitaka jumuiya ya kimataifa kugharimia shughuli hizo za kulinda amani.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya amewatuma mawaziri waandamizi kwenda nchi kadhaa za Kiafrika kutaka uungaji mkono wa uwekaji wa vikosi hivyo nchini Somalia.

Kibaki hivi sasa ni Mwenyekiti wa Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali ya Afrika IGAD ambayo hapo mwaka 2004 ilisaidia kufikiwa mwa makubaliano ya kuundwa kwa serikali ya mpito ya nchi hiyo iliochukuwa madaraka mjini Mogadishu mwezi uliopita kwa msaada wa vikosi vya Ethiopia.