1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Makaazi ya Rais Yusuf yashambuliwa kwa mizinga

20 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCZb

Kumetokea mashambulizi ya mizinga dhidi ya makaazi ya Rais wa mpito wa Somalia Abdulahi Yusuf Ahmed hapo jana wakati Umoja wa Afrika ukiwa umekubali kuweka kikosi cha kulinda amani katika nchi hiyo iliothirika na vita ambacho kimekuwa kikijadiliwa kwa muda mrefu.

Takriban makombora kumi yaliovurumishwa kwa mizinga yalishambulia Villa Somalia kusini mwa Mogadishu kabla ya vikosi vya Ethiopia ambavyo hivi karibuni vilisaidia serikali ya Yusuf kuwatimuwa Waislamu wa siasa kali kutoka Mogadishu kukimbizwa kwenye eneo hilo kuzima shambulio hilo kwa kupambana na washambuliaji.

Hakuna taarifa zilizopatikana mara juu ya majeruhi katika eneo hilo ambapo Rais Yusuf amehamia hivi karibuni na haijulikani iwapo rais huyo alikuwako ndani ya jengo hilo wakati wa shambulio hilo.

Wakati huo huo kufuatia mkutano wake mjini Addis Ababa Umoja wa Afrika umekubali uwekaji wa haraka wa kikosi cha kulinda amani cha wanajeshi 8,000 nchini Somalia ambapo dhima yake itakuwa kurahisisha operesheni za misaada ya kibinaadamu na kuimarisha amani na utulivu nchini humo.

Hadi sasa ni Uganda tu iliotangaza hadharani kwamba iko tayari kuchangia wanajeshi wake kwa kikosi hicho nchini nyengine ambazo yumkini zikachangia wanajeshi ni Nigeria,Libya na Algeria.