1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Umoja wa Afrika yatathmini usalama

27 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBMA

Timu ya wataalamu wa kijeshi ya Umoja wa Afrika imewasili katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu uliokumbwa na umwagaji damu hapo jana kutathmini shughuli za kulinda amani za Umoja wa Afrika wakati shirika moja la haki za binaadamu likirepoti kwamba watu 10 wameuwawa katika kipindi cha masaa 24.

Safari hiyo inatowa fursa kwa nchi zinazotaka kutuma vikosi vyao nafasi ya kujionea wenyewe hali ya usalama mjini Mogadishu.

Kwa mujibu wa Meja Generali Benon Biraro wa Uganda anayeongoza timu hiyo maafisa hao wamekwenda kuangalia hali ilivyo na kurepoti kwa nchi zao juu ya uwezekano wa kuwekwa kwa vikosi kutoka Afrika.

Timu hiyo pia itajadili na maafisa wa serikali iwapo mkutano wa usuluhishi wa kitaifa uliomalizika hivi karibuni umetowa matokeo yoyote yale mazuri kuboresha hali ya usalama mjini Mogadishu.