1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Wafanyikazi wasiopungua watano wauwawa kwenye mlipuko

26 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBo9

Wafanyikazi wa kike wasiopungua watano wameuwawa wakati bomu lililokuwa limetegwa kwenye jaa la takataka lililolipuka hii leo kwenye soko la Bakara mjini Mogadishu nchini Somalia.

Wanawake hao walikuwa wakifanya kazi ya kufagia katika soko hilo.

Duru za hospitali kuu ya Medina mjini Mogadishu zinasema watu wengine 10 wamejeruhiwa kwenye mlipuko huo wengine wakiwa katika hali mahututi.

Isha Hassan, mmoja wa wafanyikazi aliyeponea chupu chupu mlipuko huo, amesema bomu hilo limewalipua wenzake wanne vipande vipande.

Afisa wa polisi aliyeshuhudia mlipuko huo amesema bomu hilo huenda lilitegwa na wanamgambo wa kiislamu waliosalia mjini Mogadishu tangu walipofukuzwa na majeshi ya serikali ya mpito ya Somalia yakisaidiwa na majeshi ya Ethiopia.

Machafuko mjini Mogadishu yameendelea kuongezeka huku wanamgambo wakiwashambulia wanajeshi wa Ethiopia, maafisa wa serikali na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika karibu kila siku.