1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Wasomali watakiwa wawasilishe silaha zao

2 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCdw

Waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia, Ali Mohamed Gedi, amewataka wasomali wote wawasilishe silaha zao katika muda wa siku tatu. Bwana Gedi aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Mogadishu hapo jana.

Serikali ya mpito ya Somalia pia imeahidi msamaha kwa wanamgambo wa mahakama za kiislamu watakaoweka silaha zao chini na kujisalimisha.

Licha ya ushindi wa kijeshi dhidi ya wananamgambo wa kiislamu serikali imesema inatambua umuhimu wa suluhisho la kisiasa ili kuzuia upinzani wa kiislamu. Waziri wa mambo ya ndani wa serikali ya mpito ya Somalia, Hussein Mohammed Farah Aideed, alisema ipo haja ya kuelewana na wanamgambo wa mahakama za kiislamu ili kuzuia kuzuka upinzani kama ule wa Irak.

Hapo awali wanamgambo hao waliitoroka ngome yao ya mwisho karibu na mji wa bandari wa Kismayu kusini mwa Somalia. Duru zinasema walielekea mpaka wa Kenya huku wanajeshi wa Somalia na Ethiopia wakiwaandama.