1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Watu 200 wauwawa katika mapigano mapya

31 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCDx

Hali katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu inazidi kuwa mbaya baada ya waasi kuidungua helikopta ya kivita ya Ethiopia hapo jana na Ethiopia kusema kwamba imewauwa waasi 200 katika mapigano makali ya siku mbili kati ya vikosi vya serikali vinavyosaidiwa na Ethiopia na waasi wa Kiislam na wanamgambo wa kikabila.

Wafanya kazi wa misaada wanasema raia wengi pia wameuwawa katika mapigano hayo makali kuwahi kushuhudiwa kwa miaka mingi mjini humo na tokea kutimuliwa kwa wanamgambo wa Kiislam mjini humo mwezi wa Desemba mwaka jana na vikosi vya serikali ya mpito ya Somalia vikisaidiwa na vile vya Ethiopia.

Tume ya wakimbizi ya Umoja wa Mataifa inakadiria kwamba watu 12,000 wameukimbia mji mkuu huo wiki iliopita kuepuka umwagaji damu na kufanya idadi ya watu walioukimbia mji huo kuanzia mwezi wa Februari kufikia 57,000.