1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Watu watatu wauwawa

6 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCLj

Watu watatu wameuwawa leo nchini Somalia wakati wa ufayatulianaji wa risasi kati ya majeshi ya Ethiopia na wapiganaji ambao hawakutambuliwa.

Walioshuhudia wanasema mapigano hayo yametokea karibu na kambi ya kijeshi mjini Mogadishu saa chache baada ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika kuwasili mjini humo. Mauaji hayo yamefanyika karibu na jengo lililokuwa zamani makao makuu ya wizara ya ulinzi ambalo linatumiwa na majeshi ya Ethiopia.

Kikosi cha kwanza cha wanajeshi wa Umoja wa Afrika kutoka Uganda kiliwasili leo mjini Mogadishu kuanza kibarua chao kigumu cha kulinda amani nchini humo.

Kamishna wa amani na usalama wa Umoja wa Afrika, Said Djinnit, amesema leo ni siku ya kwanza ya kupeleka majeshi ya kulinda amani Somalia.

´Tume yetu imeenda Somalia kuwasaidia Wasomali wote na kuzisaidia juhudi za kisiasa kwa sababu hakuna chaguo lengine la harakati ya kisiasa kwa njia ya mdahalo na maridhiano. Kwa hilo kufanyika kama ilivyotaka serikali ya mpito, serikali hiyo inahitaji msaada mkubwa kutoka kwa Umoja wa Afrika.´

Habari zaidi zinasema mashambulio ya makombora yalifanywa leo katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Mogadishu.

Hakuna ripoti zozote za majeruhi zilizotolewa katika mashambulio hayo yaliyofanywa muda mfupi baada ya wanajeshi wa Uganda kuwasili mjini humo.