1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Ghasia Mogadishu

12 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCAa

Takriban watu wanne wameuawa hapo jana katika mapigano mapya mjini Mogadishu kati ya majeshi ya Ethiopia na wapiganaji wa mahakama za kiislamu.Mapigano hayo yanatokea wakati makubaliano ya muda ya kusitisha vita yalifikiwa juma moja lililopita.

Milio ya risasi na silaha nzito nzito ilisikika mitaani walikoshambuliana wapiganaji na wanajeshi hao katika mji mkuu wa Somalia.Ghasia hizo ndizo mbaya zaidi kutokea katika kipindi cha miaka 15 na kusababisha vifo vya watu alfu 1.

Viongozi wa kitamaduni wa ukoo wa Hawiye ulio na ushawishi mkubwa wanalaumu serikali kwa kuchagiza ghasia hizo zilizokiuka makubaliano ya amani yaliyodumu wiki moja.Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo na makamanda wa jeshi la Ethiopia.

Wakati huohuo Jumuiya ya Milki za Kiarabu inatangaza kuwa inaahirisha mkutano unaolenga kuleta pamoja jamii zinazohasimiana na serikali ili kutafuta amani.Mkutano huo ulipangwa kufanyika Aprili 16 na kuahirishwa hadi Mei 15 ili kuongeza muda wa matayarisho kwa mujibu wa mwakilishi wa Afrika katika Jumuiya hiyo Samir Hosni.

Mapigano makali yalizuka mwezi jana baada ya majeshi ya Ethiopia kuanzisha msako wa wanamgambo wanaolaumiwa kushambulia ngome za serikali na majeshi ya Ethiopia mjini Mogadishu.

Nchi ya Somalia imekuwa bila serikali iliyo na nguvu tangu kungolewa madarakani kwa Mohammed Siad Barre mwaka 91.

Eritrea inayohasimiana na Ethiopia kwa muda mrefu inakana kuchochea mgogoro huo wa Somalia na kutoa wito wa majeshi ya kigeni kuondoka nchini humo kikiwemo kikosi cha Umoja wa Afrika kwa madai kuwa yanachagiza hali yote.Majeshi ya Uganda pekee ndiyo yaliyoko Somalia katika mpango huo wa Umoja wa Afrika.