1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Mahakama za kiislamu zatisha kuanzisha Jihad

7 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCll

Mahakama za muungano za kiislamu nchini Somalia zinatisha kuzidisha mashambulio dhidi ya serikali baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha hatua ya kupeleka kikosi cha usalama nchini humo.Hali ni tete hivi sasa huku mapigano yakiendelea kati ya makundi tofauti yanayoungwa mkono na majeshi ya Ethiopia katika ya Somali.

Mpiganaji mmoja anayeunga mkono serikali ameripotiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa.Kulingana na msimamizi wa masuala ya usalama katika mahakama hizo za kiislamu Sheikh Mukhtar Robow,Baraza hilo linatekeleza matakwa ya Marekani kwani hawajahusishwa.

Serikali ya Somalia kwa upande wake inakubali hatua hiyo ya kupeleka majeshi kutoka mataifa jirani ya Afrika kwani inashindwa nguvu na mahakama za kiislamu.Mahakama hizo zinadhibiti maeneo mengi nchini humo kwa sasa.

Azimio hilo linaloungwa mkono na wanachama wa Baraza hilo kutoka mataifa ya Kongo,Tanzania na Ghana linaondoa vikwazo vya silaha ilivyowekewa Somalia mwaka 92.Hatua hiyo itakiwezesha kikosi hicho cha wanajeshi alfu 8 kupewa silaha aidha kutoa mafunzo kwa majeshi ya usalama ya serikali.

Kwa upande mwingine azimio hilo linatisha kuwekea vikwazo wahusika wengine ambao watakiuka makubaliano hayo na kutoa wito kwa wapiganaji wa kiislamu kusitisha mapigano na kuungana na serikali ya muda ya Somalia ili kuafikiana.

Nchi ya Uganda kupitia Waziri wake wa Ulinzi Ruth Nankabirwa imetangaza kuwa iko tayari kupeleka kikosi cha kulinda amani nchini Somalia kufuatia uamuzi huo