1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Wanamgambo si kitisho tena kwa serikali

24 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBfi

Meya mjini Mogadishu nchini Somalia Mohamed Omar Habeb anasema kuwa wanamgambo wanaoshambulia serikali wanatoroka na si kitisho tena.Mapema mwaka huu jeshi la serikali ya Somalia likungwa mkono na majeshi ya Ethiopia walifurusha wapiganaji wa mahakama za kiislamu walioteka sehemu kubwa ya nchi hiyo.Wanamgambo wanaripotiwa kushambulia serikali ya muda ya Somalia aidha vikosi vya Ethiopia na Umoja wa Afrika vinavyolinda usalama.

Hata hivyo ghasia zimepungua katika kipindi cha siku kadhaa zilizopita baada ya operesheni ya polisi ya kuwasaka wanamgambo hao.Madhumuni ya operesheni hiyo ni ya kudumisha usalama wakati wa mkutano wa kutafuta amani ya Somalia uliokwama kwasababu za kiusalama.

Serikali ya Somalia inalaumiwa kusababisha uhasama na wapiganaji wa Kiislamu kwa kuanzisha mkutano wa maridhiano bila kuwashirikisha wapinzani wake wakuu.