1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Wapiganaji wakiislamu wakubali mazungumzo na serikali ya mpito Somalia

6 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCvh

Wapiganaji wa mahakama za kiislamu nchini Somalia wamekubali hapo jana kuwa na mazungumzo mengine ya amani na serikali ya mpito.

Hatua hii imefuatia ziara ya dharura ya spika wa bunge Sharif Hassan Sheikh Aden ya kuwashawishi wapiganaji hao wanaoyashikilia maeneo mengi ya Somalia ukiwemo mji mkuu Mogadishu.

Bwana Aden alikutana jana na wapiganaji wa mahakama za kiisalmu licha ya wito wa serikali ya mpito wa kutaka asifanye hivyo.

Hata hivyo hakuna matumaini kamili ya kufufuka kwa duru ya tatu ya mazungumzo hayo ya amani ambayo yalivunjika wiki iliyopita huko Sudan.

Hii inatokana na pande zote mbili serikali ya mpito na kundi hilo na wapiganaji wa mahakama za kiislamu kuendelea kujitaarisha kwa vita ambavyo vinahofiwa na wengi huenda vikalitumbukiza eneo la upembe wa Afrika kwenye ghasia.

Wapiganaji wa mahakama za kiisalmu wametoa sharti la kukutana ana kwa ana na serikali ya mpito lakini hakuna tamko lolote lililotolewa na upande wa serikali kuhusiana na suala hilo.

Jana jumapili wakaazi wa nje ya mji wa Baidoa wamesema kumekuwepo na milio ya risasi kwenye eneo hilo.