1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mogherini akutana na Netanyahu na Abbas

21 Mei 2015

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini anaendelea na ziara yake ya Mashariki ya Kati. Jana (20.05.2015) alikutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas.

https://p.dw.com/p/1FTW7
Israel Jerusalem Mogherini bei Netanjahu
Mogherini na Netanyahu mjini JerusalemPicha: Reuters/Dan Balilty

Mogherini alisisitiza uhusiano wa karibu kati ya Israel na Ulaya na kumhakikishia Netanyahu kwamba Umoja wa Ulaya umejitolea kwa dhati kuizuia Iran isitengeneze silaha za nyuklia. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Jerusalem akiwa pamoja na Netanyahu, Mogherini alisisitiza msaada wa Ulaya katika juhudi za kuundwa taifa huru la Palestina kabla kufanya kikao cha faragha na waziri mkuu huyo wa Israel.

"Naamini ahadi yako ya kujitolea tena kushughulikia amani na usalama kwanza kwa Israel, lakini pia kwa eneo zima, ni jambo linalotuunganisha sote. Umoja wa Ulaya unataka amani kwa Israel na eneo hili kwa sababu hii pia ni muhimu kwa amani na usalama wa Ulaya. Tuna vitisho vingi tunavyolazimika kuvikabili kwa pamoja."

Netanyahu alitumia fursa hiyo kuzungumzia baadhi ya ukosoaji unaotolewa dhidi ya serikali yake mpya. "Israel inataka amani, mimi nataka amani. Tunataka amani itakayoumaliza mzozo huu kabisa. Msimamo wangu haujabadilika; siungi mkono suluhisho la taifa moja, siamini hilo ndilo suluhisho. Naunga mkono suluhisho la mataifa mawili, taifa la Palestina lisilo silaha linalolitambua taifa la kiyahudi."

Matamshi ya Netanyahu yalionekana kupingana na kauli aliyoitoa miezi miwili iliyopita kuhusu suala hilo. Kiongozi huyo aliikasirisha Marekani na washirika wengine muhimu wakati wa kampeni ya uchaguzi mwezi Machi kwa kusema hatoruhusu kuundwa kwa taifa la Palestina akiwa madarakani, ingawa baadaye alijaribu kubadili msimamo wake.

Mogherini akutana na Abbas

Umoja wa Ulaya umekosoa vikali ujenzi wa makazi ya walowezi wa kiyahudi katika eneo la Ukingo wa Magharibi, huku baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo zikilazimisha bidhaa zinazozalishwa katika makazi hayo ziwe na vitambulisho maalumu ili ziweze kuuzwa Ulaya.

Israel Jerusalem Mogherini bei Abbas
Mogherini na Abbas mjini RamallahPicha: Getty Images/AFP/A. Momani

Awali jana Mogherini alikutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas katika mji wa Ramallah, huko Ukingo wa Magharibi, kituo chake cha kwanza cha ziara ya siku mbili Mashariki ya Kati kujadili uwezekano wa kupatikana amani kati ya Israel na Wapalestina.

Miezi sita tangu alipochukua wadhifa wake, waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Italia mwenye umri wa miaka 41 anataka kuimarisha nafasi ya Ulaya kama mshirika mkubwa wa kibiashara wa Israel na mfadhili mkubwa wa Wapalestina baada ya Marekani kushindwa mwaka jana kupata ufanisi katika juhudi mpya za kutafuta amani kati ya pande hizo mbili.

Mogherini amesema Umoja wa Ulaya utafanya kila linalowezekana kuyaufua tena mazungumzo ya amani yaliyovunjika mwaka jana. Mpatanishi wa Palestina katika mazungumzo hayo Saeb Erakat alimkaribisha Mogherini na kuitaka Israel iache kupanua ujenzi wa makazi ya walowezi Ukingo wa Magharibi na iwaachie huru wafungwa wa Kipalestina.

Hii ni ziara ya kwanza ya Mogherini katika eneo hilo tangu serikali mpya ya Israel ilipoapishwa wiki iliyopita. Mogherini anatarajiwa kukutana na rais wa Israel Reuven Rivlin na kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo Isaac Herzog hivi leo.

Mwandishi: Josephat Charo/DPA/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef