1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MONROVIA:Kansela Merkel atoa mwito Liberia ifutiwe madeni

8 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Hh

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekamilisha ziara yake katika nchi tatu za Afrika kwa kuitembelea Liberia.

Akiwa mjini Monrovia kansela Merkel alifanya mazungumzo na mwenyeji wake rais Ellen Johson Sirleaf.

Katika ziara hiyo ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi wa kiserikali ya Ujerumani kansela Angela Merkel amesema ziara yake katika nchi hiyo ililenga kumuunga mkono rais wa kwanza wa kike barani Afrika.

Bibi Merkel amesema amefurahi kupata fursa ya kuitembelea Liberia ambapo amejionea uharibifu mkubwa uliosababishwa na vita.

Amesema nchi hiyo ina vijana wengi walio chini ya umri wa miaka 20 kwa hivyo iwapo hawatapewa matumaini ya haraka basi kuna hatari ya kutokea vurugu na hilo lazima lizuiwe.

Ujerumani imeahidi msaada wa Euro milioni nne zaidi kwa ajili ya ujenzi wa taifa hilo. Kabla hajaanza ziara yake akiwa mjini Berlin bibi Merkel alishuhudia kuidhinishwa msaada wa Euro milioni 14.4 kwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Bibi Merkel pia ametoa mwito wa kuondolewa mzigo wa madeni serikali ya Liberia.