1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morgan Tsvangirai ameapishwa Waziri Mkuu wa Zimbabwe

C.Stäcker - (P.Martin)11 Februari 2009

Nchini Zimbabwe,kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai ameapishwa Waziri Mkuu na hivyo kuungana na Rais Robert Mugabe katika serikali ya umoja wa kitaifa.

https://p.dw.com/p/GrWw

Hata hivyo ni wachache mno wanaoamini kuwa Tsvangirai ataweza kutekeleza mapendekezo yake mbele ya Mugabe.Morgan Tsvangirai,kongozi wa chama cha Movement for Democratic Change-MDC- anatambua kitisho cha kumezwa na chama cha ZANU-PF kama mahasimu wa zamani wa Mugabe,bila ya kubadilisha mkondo unaofuatwa na taifa linalosambaratika.Kwani Tsvangirai si kiongozi wa serikali mpya ya mpito.

Yeye ana haki ya kutoa mapendekezo na wakati mwingine kumwakilisha Mugabe anaebakia rais licha ya kushindwa uchaguzi uliofanywa mwezi wa Machi mwaka 2008.Kwa hivyo Mugabe ni kiongozi wa serikali na vile vile mkuu wa Tsvangirai.Na hiyo huwatia wasiwasi Wazimbabwe wengi. Mmoja wao ni mwanaharakati wa haki za binadamu Tsitsi Torongo mwenye miaka 29.Yeye anasema:

"Mimi binafsi kamwe sijawahi kukiamini chama cha ZANU-PF.Hofu yangu ni kuwa wataendelea kuizuia serikali hiyo kufanya kazi yake na hivyo kuzuia masuala muhimu kushughulikiwa kama ipasavyo."

Hata Clever Bere,Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Zimbabwe -ZINASU- ana hofu zake kuhusu serikali mpya mpito.Hata hivyo,anasema serikali hiyo ya mpito ipewe muda.Akaongezea:

"Hatuuamini muundo wa serikali.Labda tunahitaji kuipa muda na kuipima serikali hiyo kwa kile kitakachotekelezwa.Maoni yetu ni kuwa hiyo ni serikali ya mpito na kazi yake ni kushughulikia masuala muhimu yanayohitaji kushughulikiwa wakati huo wa mpito."

Licha ya hofu zao,Wazimbabwe wengi wanahisi kuwa serikali hiyo ya mpito ni njia pekee ya kusonga mbele.Morgan Tsvangirai amesema,huu ni wakati wa kihistoria.Kwa kweli kisiasa,Tsvangirai hakuwa na chaguo jingine. Kwa maoni ya mchambuzi huru wa masuala ya kisiasa nchini Afrika Kusini Daniel Silke,kuingia madarakani kwa Morgan Tsvangirai ni hatua muhimu katika kurejesha hali ya kawaida nchini Zimbabwe.