1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morocco washinda kombe la CHAN 2018

Bruce Amani
5 Februari 2018

Morocco imekuwa nchi ya kwanza mwenyeji kutwaa kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani – CHAN: Iliilaza Nigeria mabao manne kwa sifuri katika fainali ya mjini Casablanca

https://p.dw.com/p/2s9rm
Afrikanische Nationenmeisterschaft 2018 Marokko - Nigeria
Picha: Getty Images/AFP/F. Senna

Morocco iliinyuka Nigeria mabao manne kwa sifuri katika fainali ya Jumapili usiku mjini Casablanca. Mchezaji wa Morocco Zakaria Hadraf alifanikiwa kupachika wavuni bao la kwanza muda mfupi kabla ya kipindi cha mapumziko huku mchezaji wa Nigeria Peter Eneji Moses akitimuliwa uwanjani baada ya kupewa kadi ya pili ya njano

Walid El Karti na Hadraf - katika bao lake la pili - waliipatia Morocco uongozi katika mechi hiyo kufikia dakika sitini. Ayoub El Kaabi, afanikiwa kulifunga bao lake la tisa katika mashindano hayo ya Afriak kwa wachezaji wa ligi za nyumbani

Sudan ilifanya vizuri na kumaliza katika nafasi ya tatu katika dimba hilo baada ya kuipiku Libya. Morocco pia ndio mabingwa wa kwanza kushinda mechi tano kati ya sita – baada ya kuwalaza Mauritania, Guinea, Namibia na Libya kabla ya kuwanyeshea mvua ya magoli Nigeria.

Kocha wa Morocco Herve Renard sasa atawaandaa vijana wake kupambana na Iran, Ureno na Uhispania katika Kombe la Dunia baadaye mwaka huu nchini Urusi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba