1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morocco yaaga mashindano kwa pambano dhidi ya Niger

Sekione Kitojo30 Januari 2012

Fainali zinazoendelea za kombe la mataifa ya Afrika huko Guinea ya Ikweta na Gabon , Senegal iliyopigiwa upatu kuwa ni moja ya timu zinazotarajiwa kutoroka na kombe hilo yaambulia patupu.

https://p.dw.com/p/13t8v
Orange Africa Cup of Nations. Die 28. Fußball-Afrikameisterschaft 2012 (Africa Cup oder engl.: Africa Cup of Nations), organisiert vom afrikanischen Verband Confédération Africaine de Football (CAF), findet in Gabun und Äquatorialguinea statt.[1] Wie bei der vergangenen Afrikameisterschaft treten zusammen mit den Gastgebern 16 Mannschaften zunächst in Gruppen und danach in Ausscheidungsspielen gegeneinander an. Insgesamt werden 32 Spiele ausgetragen.
Nembo ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika

Jana Zambia ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wenza wa mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika dhidi ya Guinea ya Ikweta na kushika usukani wa kundi A. Alikuwa sajini wa zamani wa jeshi la Zambia , Christopher Katongo aliyeunyamazisha umati wa mashabiki wa Guinea ya Ikweta na kuiweka timu hiyo ya kusini mwa Afrika katika nafasi ya kwanza katika kundi hilo ikiwa na points 7, wakati Guinea ya Ikweta hata hivyo ilikwisha fuzu kuingia katika duru ya mtoano ya timu nane.

Libya ambayo imeishinda Senegal kwa mabao 2-1 mjini Bata , imemaliza ikiwa na points 4, wakati Senegal imeambulia patupu, haikupata hata point moja. Hali hii imewashangaza wachambuzi wengi wa masuala ya soka barani Afrika na duniani, kwani Senegal ilitarajiwa kufanya makubwa katika fainali hizi, hasa ikitiliwa maanani uwezo mkubwa wa mashambuliaji wake kama Demba Ba, Papis Demba Cisse, na Mussa Sow. Lakini silaha hizo zilishindwa kuripuka mbele ya risasi za rashasha za Chipolopolo , Zambia, Libya na hata wenyeji wenza wa mashindano haya Guinea ya Ikweta ambayo iko katika nafasi ya 151 katika orodha ya timu bora ya shirikisho la soka duniani la FIFA.

Nae kocha wa Morocco Eric Gerets , katika kile kinachoonekana kama mchezo wake wa mwisho akiwa na timu hiyo , atawatarajia wachezaji wake waache hali yao ya kujikunyata katika fainali hizo nchini Gabon kwa kupata ushindi katika pambano lao na Niger hii leo. Pande zote mbili zinaelekea nyumbani baada ya mchezo huu wa kundi C katika fainali za kombe la Afrika baada ya kupata vipigo na kuzuwia nia yao ya kuingia katika robo fainali , dhidi ya wenyeji wenza wa mashindano haya Gabon na Tunisia.

Tunisian teammates, including Aymen Abdennour (Top) embrace goalscorer Youssef Msakni (hidden) during the Africa Cup of Nations match between Morocco and Tunisia in Libreville, Gabon, 23 January 2012. EPA/STR EDITORIAL USE ONLY
Timu ya taifa ya Tunisia wakishangiria bao dhidi ya Morocco.Picha: picture-alliance/dpa

Wakati ni heshima tu iliyobaki kulindwa katika mchezo huo , inaelekea mchezo huo utakuwa mgumu ,ambapo Niger itataka kupata point za kwanza katika fainali hizi , na Gerets anamatumaini kuwa timu yake itaonyesha mchezo mzuri ambao utaweza kuwashawishi waajiri wake kuwa anastahili mshahara wake wa euro laki mbili kwa mwezi.

Baada ya kupata kipigo cha mabao 3-2 siku ya Ijumaa dhidi ya Gabon ambacho kilifunga ukurasa wa Morocco katika mashindano haya kocha huyo wa zamani wa timu ya daraja la kwanza nchini Ufaransa , Marseille , alijifungia katika chumba chake cha hoteli, akitafakari hatima yake.

Jioni ya Leo Niger itaonyeshana kazi na Morocco wakati wenyeji Gabon watakuwa na miadi na Tunisia , timu hizo zikitafuta kuamua nani anashika nafasi ya kwanza na nani wa pili kuelekea katika duru ya mtoano ya timu nane.

Na katika ligi ya Ujerumani , Bundesliga , mpambano kuelekea ubingwa unabakia kuwa wenye msisimko mkubwa , ambapo Bayern Munich ambayo inaendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi iliweza kupata ushindi dhidi ya Wolfsburg na pia Borussia Dortmund na Schalke 04 ziliiweza kupata ushindi, na kuwa sawa kwa points na Bayern. Lakini hata Borussia Moenchengladbach ilifanikiwa kupata ushindi katika mchezo wa mwisho jana wa kukamilisha duru ya 19 ya ligi hiyo.

Katika mchezo huu wa 19 bado timu tatu zimefungana kwa points. Bayern Munich baada ya kufanya kazi ya ziada iliweza kupata ushindi muhimu dhidi ya Wolfsburg kwa mabao 2-0. Mfungaji wa bao la pili Arjen Robben anasemakuwa na hapa namnukuu,

"Huenda ulikuwa si mchezo mzuri , lakini tumeona kwamba kulikuwa na hali bora kiasi katika mchezo wetu. Kutokana na hali hiyo tunapaswa kufanyia kazi zaidi mchezo. Leo tulicheza kwa kupambana zaidi".

Borussia Dortmund ambayo iko sawa kwa points na Bayern Munich ,zote zina points 40, ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Hoffenheim. Uchezaji wa timu hiyo unaweza kuwa bora zaidi, ameeleza mshambuliaji wa mabingwa hao watetezi Borussia Dortmund Kevin Großkreutz.

"Nafikiri , tungeweza kupandisha zaidi kiwango chetu. Katika kipindi cha kwanza tumeonyesha mchezo mzuri na kupata mabao 3. Katika kipindi cha pili tulilegea kidogo. Hali hii haingepasa kuwa. Kwa goli lililofungwa dhidi yetu ni makosa yetu. Tungeweza kufanya vizuri zaidi".

Schalke 04 iliishinda FC Koln kwa mabao 4-1 , wakati Borussia Moenchengladbach iliishinda VFB Stuttgart kwa mabao 3-0. Nayo Mainz 05 ikapata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya timu iliyoko katika hatari ya kushuka daraja ya Freiburg ambayo mshambuliaji wake hatari Papis Demba Sisse ameiacha mkono na kujiunga na Newcastle ya Uingereza hivi karibuni.

Wakati huo huo nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani Michael Ballack , hatima yake katika timu ya Bayer Leverkusen haijulikani baada ya afisa mtendaji Wolfgang Holzhaeuser kusema kuwa timu hiyo inajitayarisha kumuuza kabla ya dirisha dogo la uhamisho kufungwa hapo kesho Jumanne.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 alikuwa katika benchi wakati wa pambano la timu hiyo na Werder Bremen ambapo timu hizo zilitoshana sare ya bao 1-1. Mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu. Licha ya kuwa amecheza mara 14 katika michezo 18 ya Leverkusen katika ligi ya Ujerumani msimu huu , ni michezo mitano tu ambayo amecheza kwa muda wa dakika zote 90, na Ballack ambaye ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mara 98, si mgeni na kukaa benchi katika timu hiyo ya Leverkusen.

Na kwa taarifa hiyo sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo kwa leo na hadi mara nyingine jina langu ni Sekione Kitojo , nasema kwaherini.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / afpe

Mhariri : Yusuf Saumu.