1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MORONI : Duru ya pili ya uchaguzi wa rais Comoro

24 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBor

Visiwa viwili vya Comoro vya Ngazija na Moheli leo hii vinapiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa marais wa serikali ya shirikisho bila ya kisiwa cha tatu cha Anjouan ambacho uchaguzi wake umetangazwa kuwa batili na haufai na Umoja wa Afrika.

Upigaji kura katika mji mkuu wa Moroni umekuwa ukifanyika kwa utulivu licha ya kuchelewa kuanza.

Katika kisiwa kikuu cha Ngazija marudio ya uchaguzi huo ni kati ya hakimu mwenye umri wa miaka 48 Mohamed Abdoulwahabi na mwanasheria Mkomoro wa Ufaransa Said Larifou baada ya rais anayeondoka madarakani wa kisiwa hicho Abdou Soule Elbak kushindwa katika duru ya kwanza.

Katika kisiwa cha Moheli Mohamed Ali Said ambaye alikuwa anaongoza katika duru ya kwanza ya uchaguzi hapo tarehe 10 mwezi wa Juni anawania urais huo dhidi ya kiongozi alieko madarakani Said Mohamed Fazul.

Uchaguzi huo huafanyiki katika kisiwa cha Anjouan ambacho kilifanya uchaguzi huo kwa kukaidi amri ya serikali kuu ya taifa ya kuuahirisha uchaguzi huo kutokana na wasi wasi wa usalama.

Umoja wa Afrika umeupuuzilia mbali uchaguzi huo na kumuamuru kiongozi wa zamani wa kisiwa hicho Mohamed Bakar kuitisha uchaguzi mpya.

Hata hivyo Bakar ambaye katika uchaguzi huo alichaguliwa kuwa rais ametangaza baraza la mawaziri la watu 10 na kuuambia Umoja wa Afrika uwachae kutia mafuta kwenye moto.