1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morsi akatalia madarakani

3 Julai 2013

Mvutano nchini Misri wazidi kurindima,jeshi liko tayari kuangamia kuilinda nchi wakati rais Morsi akitangaza kuwa tayari kujitowa muhanga kulinda madaraka yake

https://p.dw.com/p/191iV
Mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Sisi rais Mohamed Morsi
Mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Sisi rais Mohamed MorsiPicha: Reuters

Taarifa zinasema rais Morsi amepigwa marufuku kusafiri kokote nje ya nchi huku ikitajwa kwamba jeshi linajiandaa kuyatibua maandamano ya wafuasi wa rais huyo. Muda wa saa kadhaa zilizopita 03.07.2013 Jeshi lilitowa mwito uliopewa kichwa cha maneno mwito wa dakika za lala salama,likisema liko tayari kumwaga damu dhidi ya magaidi na wapumbavu baada ya rais Morsi kukataa kuachia ngazi.

Viongozi wa kijeshi wameapa kwa hivyo kurudisha hali ya kawaida katika taifa hilo lililogubikwa na maandamano ya kupinga sera za rais Morsi za itikadi kali.Wakati wowote kutoka sasa jeshi linatazamiwa kuchukuwa uamuzi wake wa mwisho katika mvutano huo,hatua ambayo wengi wanahisi itakuwa ni ya mapinduzi yanayoungwa mkono na waandamanaji katika uwanja wa Tahrir wanaompinga Morsi na chama chake cha Udugu wa Kiislamu.

Maandamano ya kumpinga Mosri uwanja wa Tahrir
Maandamano ya kumpinga Mosri uwanja wa TahrirPicha: Getty Images

Kwa upande mwingine Morsi lakini amependekeza kuwa tayari kukubali serikali ya maridhiano.Awali lakini msemaji wa rais huyo alisema kiongozi huyo ameapa kwamba ni bora apoteze maisha yake akitetea demokrasia kuliko kulaumiwa katika kumbukumbu za historia.

Wasiwasi umetanda kote katika taifa hilo huku duru za usalama zikisema magari mawili yaliyosheheni wanajeshi yameshakita kambi nje ya makao makuu ya shirika la utangazaji la serikali na wengi wa wafanyakazi wa shirika hilo wametimuliwa kutoka jengo hilo.Taarifa nyingine zilizotangazwa na shirika la habari la Mena limesema wafanyikazi wa serikali wameivamia ofisi ya waziri mkuu na kumzuia waziri mkuu Hisham Kandil kutoingia ofisi hizo.Msemaji wa chama cha Udugu wa Kiislamu cha rais Morsi amesema wafuasi wa rais huyo wako tayari kufa mashahid kwa kumlinda kiongozi huyo.Kila mmoja anasubiri kusikia kauli ya jeshi ambalo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Facebook linatajwa hivi sasa kukutana na viongozi wa kidini,kisiasa na makundi ya vijana.Taarifa hiyo imesema mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Sisi atatangaza kauli ya jeshi mara tu atakapokamilisha mazungumzo na viongozi hao.

Wafuasi wa rais Mosri Cairo
Wafuasi wa rais Mosri CairoPicha: Reuters

Katika tukio la kushangaza,Chombo kikuu cha kihseria nchini humo imethibitisha kumrudisha mwendesha mashtaka mkuu wa serikali Abdel Meguid Mahmoud tukio linalomshinikiza zaidi rais Morsi aliyemtimua kazini Novemba mwaka jana.Baraza kuu la sheria limechukua hatua hiyo siki moja baada ya mahakama ya rufaa kutowa uamuzi wa mwisho wa kutaka Mahmud arudishwe kazini.

Mwandishi:Yusuf Saumu/Reuters/Dpa

Mhariri:Josephat Charo