1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Morsi awaonya raia Misri"

Admin.WagnerD27 Desemba 2012

Rais Mohammed Morsi wa Misri amesema zoezi la upigaji kura ya maoni kuhusu katiba mpya kwa raia wa taifa lake ulikuwa wa uwazi mkubwa chini ya usimamizi wa vyama vya kiraia pamoja na mahakama

https://p.dw.com/p/179Od
In this image released by the Egyptian Presidency, President Mohammed Morsi prepares to make a televised address to the nation in Cairo, Egypt, Wednesday, Dec. 26, 2012. Morsi says the new constitution establishes Egypt's new republic, calling on opposition to join dialogue to heal rifts and shift the focus toward repairing the economy.(Foto:Egyptian Presidency/AP/dapd)
Rais Mohammed Mursi wa MisriPicha: AP

Rais Mohammed Morsi wa Misri amesema zoezi la upigaji kura ya maoni kuhusu katiba mpya kwa raia wa taifa lake ulikuwa wa uwazi mkubwa chini ya usimamizi wa vyama vya kiraia pamoja na mahakama huku akitaka vyama vyote nchini humo kuungana naye katika mjadala wa maendeleo ya kitaifa.

Akizungumza kupitia televisheni katika hotuba yake kwa umma wa Wamisri muda mfupi baada ya kutia saini mapendekezo hayo kuwa sheria kamili, Morsi alisema anarejea tena wito wake wa kuvitaka vyama vyote vya siasa pamoja na vyombo vingine vya dola kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa.

Katika hotuba yake hiyo rais Morsi aliendelea kusema ni kweli kuwa kuna mapungufu na mianya kadhaa lakini Mungu anajua kwa kuwa kila hatua anayoichukua ni kwa ajili ya taifa hilo.

Rasimu ya katiba hiyo iliyoundwa na jopo linaloongozwa na waislamu wa chama cha udugu wa kiislamu ilipitishwa kwa asilimia 63.8 ya kura kwa mujibu wa matokeo yaliotangazwa Jumanne iliyopita.

Upinzani wapinga matokeo

Wapinzani wa Morsi wanasema sheria hiyo mpya inaegemea zaidi upande wa Uislamu na kwamba haioneshi maana halisi ya mageuzi yaliyomuondoa madarakani rais wa zamani wa taifa hilo, Hosni Mubarak. Ni aslimia 33 tu ya wapiga kura ndio waliojitokeza katika zoezi hilo.

Ägypten: die politische Lage nach dem Referendum "blood will be replied by blood" als Graffiti an einer Mauer in Kairo writing in the street "blood will be replied by blood" 26-12-2012; Cairo, Egypt Foto: Korrespondent in Ägypten Nael Eltoukhy
Wapinga katiba mpya MisriPicha: DW/Nael Eltoukhy

Hata hivyo katika hotuba yake rais Morsi amesema bado anakaribisha mawazo ya wale wote waliopiga kura ya hapana katika zoezi hilo sambamba na kuwahakakishia Wamisri kwamba taifa hilo kamwe halitarejea kule lilikotokea kwa maana ya kwamba kurudia katika vurugu.

Morsi aonya raia

Pamoja na kuonya raia wa taifa hilo ambao wanajaribu kufanya mambo yatakayoweza kuhatarisha usalama wa umma amesema pia tatizo la uchumi litakuwa kipaumbele chake. Katika suala hilo alisisitiza kwamba atafanya jitihada zake zote katika kukabiliana nalo kutokana na kukabiliwa na changamoto kadhaa.

Kampuni ya kimataifa ya makadirio ya uchumi, Standard & Poor's, iliipanga Misri kwa muda mrefu katika kiwango duni cha B- huku kukiwa na shaka ya taifa hilo kutokuwa na uwezo katika kustawisha makusanyo yake ya kodi mbalimbali.

Mapema jana wanachama 90 wa kati ya 270 kutoka katika baraza madhubuti la Shura wamekula kiapo chao rasmi cha ubunge kikatiba kwa nia ya kuunda baraza la muda mfupi kwa lengo la kushughulikia masuala mbalimbali. Katiba mpya ya Misri inaruhusu baraza la Shura kufanya kazi ya bunge kwa muda ambazo awali zilikuwa katika mikono ya rais. Chombo hicho kitatekeleza majukumu yake mpaka pale bunge litakapochaguliwa.

Wanachama hao 90 walioteuliwa na Mursi mwenyewe wataungana na washauri wengine 180 walioteuliwa mapema mwaka huu. Chama cha Udugu wa Kiislamu cha Morsi na washirika wao wengine wa kiislamu wanaunda asilimia 70 ya baraza hilo.

Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Josephat Charo