1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moscow. Russia yajaribisha kombora jipya.

30 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBwm

Russia imesema kuwa imejaribisha kombora jipya ambalo litakuwa na vichwa vingi , ambalo litakuwa na uwezo wa kupenya mfumo wa aina yoyote wa ulinzi, ikiwa ni pamoja na ngao inayokusudiwa kuwekwa na Marekani katika bara la Ulaya.

Uongozi wa jeshi la Russia umesema kuwa kombora la RS-24 lilifyatuliwa kutoka katika kituo kaskazini ya mji wa Moscow na saa moja baadaye lilipiga lengo lake katika rasi ya Kamchatka katika bahari ya Pacific, umbali wa kilometa 6,000.

Utawala wa rais Bush umesema kuwa mpango wake wa kuweka ngao dhidi ya makombora, baadhi ukiwekwa nchini Poland na jamhuri ya Cheki, hauilengi Russia bali mataifa kama Iran.

Akizungumza mjini Moscow na waziri mkuu wa Ureno Jose Socrates, nchi ambayo itachukua kiti cha urais wa umoja wa Ulaya hapo Julai mosi, rais wa Russia Vladimir Putin ameonya kuwa mfumo huo wa ulinzi wa Marekani utaigeuza Ulaya kuwa majivu.