1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOSCOW: Urusi yachunguza ajali ya treni ya abiria

14 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBZD

Urusi imeanzisha uchunguzi kubaini sababu ya ajali ya treniy a abiria iliyoacha reli na mabehewa yake kadhaa kuanguka wakati ilipokuwa ikisafiri kutoka mji mkuu Moscow kwenda St Petersburg.

Maafisa wanasema madarzeni ya abiria wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo, wengine kati yao vibaya.

Akizungumza katika eneo la ajali hiyo, Sergei Wednitschenko muendeshaji mshataka mkuu wa serikali alisema, ´Ajali ya treni imesababishwa na mlipuko wa bomu lililotengenezwa nyumbani. Shirika la ujasusi FSB linachunguza kisa hicho. Tunashuku ni shambulio la kigaidi.´

Kiongozi wa shirika la ujasusi la Urusi, FSB, amesema ajali hiyo huenda imesababishwa na shambulio la waasi wa eneo la kusini mwa Urusi linalopakana na Chechnya, ambako Urusi imekuwa ikipigana vita kupinga upinzani dhidi ya utawala wake.

Lakini shirika la habari la Interfax limemnukulu mchunguzi mmoja akisema bomu lililotumiwa kufanya shambulio dhidi ya treni hiyo ni kama lile lililotumiwa na warusi wawili kulipua treni moja karibu na mji mkuu Moscow miaka miwili iliyopita.

Abiria 60 na wafanyakazi wa treni walijeruhiwa wakati treni ilipoacha reli karibu na kijiji cha Malaya Vishera, yapata kilomita 500 kaskazini mwa Moscow.