1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kuinua uchumi

Oumilkher Hamidou13 Januari 2009

Eti kitita cha yuro bilioni 50 kinatosha?Wanajiuliza wahariri wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/GXBp
Kansela Merkel akiamkiana na mkuu wa chama ndugu cha CSU,SeehoferPicha: picture-alliance/ dpa



 Mbali na mvutano wa gesi kati ya Urusi na Ukraine na maandalizi ya kuapishwa rais mteule wa Marekani Barack Obama,wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamechambua kwa marefu na mapana mpango wa serikali kuu wa kuinua shughuli za kiuchumi nchini Ujerumani.Gazeti la Schweriner Volkszeitung linaandika:


Matokeo ya mpango huu wa pili wa kunusuru uchumi mtu hawezi kuyalinganisha na mfano wa kuigizwa wa mazungumzo ya kina na uongozi madhubuti.Mvutano wa kodi ya mapato ambapo mwenyekiti wa chama cha CSU Horst Seehofer alimtia kishindo kansela Merkel aridhie madai yake,lilikua suala la fahari.Mvutano huo umewafanya watu wasahau kwamba uwekezaji katika miradi ya miundo mbinu-,ambao ndio unaogharimu fedha nyingi zaidi,haukua ukibishwa.Na suala lililozuka tangu mpango wa mwanzo wa kuinua uchumi ulipopitishwa,limejitokeza upya nalo ni kama maridhiano yaliyofikiwa yanatosha kumaliza mzozo wa kiuchumi.Uwezekano ni mkubwa kwamba hata huu hautakua mpango wa mwisho wa kuinua uchumi."



"Hata gazeti la TAGESZEITUNG la mjini Berlin linahisi matokeo ya mkutano wa jana ni haba.Gazeti linaendelea kuandika:



"Utafikiri ni  kitita kikubwa mno unaposikia serikali kuu ikizungumzia juu ya yuro bilioni 50 za kuinua shughuli za kiuchumi.Lakini kitita hicho ni cha miaka miwili.Kwa namna hiyo,mpango wa kuinua shughuli za kiuchumi unafikia asili mia moja tuu ya pato la ndani.Ni kiwango kidogo tuu hicho cha fedha.Tena kidogo sana,tukitilia maanani hali halisi namna ilivyo.Ni kiroja hiki kuona kwamba katika mzozo mkubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa,panatolewa kitita kidogo kama hicho cha fedha."



Wiki kama moja hivi kabla ya rais mteule wa Marekani kukabidhiwa hatamu za uongozi,Barack Obama ameshazungia siasa yake ya nje.Na gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linaandika:



"Hatua ya kwanza bayana anasema ni kuifunga kambi ya wafungwa ya Guantanamo.Hatua hiyo itapelekea kuitakasa upya hadhi ya Marekani,sio tuu katika eneo la Mashariki ya Kati,bali pia katika sehemu nyengine za dunia.Mzozo wa Palastina na mvutano kati ya Marekani na jamhuri ya kiislam ya Iran,na hasa mzozo uliosababishwa na mradi wake wa kinuklea ni miongoni  mwa mada zinazopewa kipa umbele katika siasa yake ya nje.Pekee ile hali ya kujiepusha na "matamshi ya ushari",kisaikolojia itaonekana kama dalili njema ya kutuliza hali ya kisiasa."