1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Kuiongoza Burkina Faso wapendekezwa

Mjahida10 Novemba 2014

Viongozi wa Vyama vya upinzani, makundi ya mashirika ya kiraia na wa kidini wamepitisha mpango wa pamoja wa kuiongoza Burkina Faso kuelekea kipindi cha mpito hadi uchaguzi mwaka ujao.

https://p.dw.com/p/1Dk3i
Ramani ya Burkina Faso
Ramani ya Burkina Faso

Hata hivyo makubaliano hayo ya pamoja kati ya upinzani, makundi ya kiraia na viongozi wa kidini yaliofikiwa jana jumapili baada ya siku kadhaa ya mazungumzo yaliofanyika mjini Ouagadougou, yanatarajiwa kuwasilishwa kwa Luteni Kanali Zida hii leo.

Mpango huo wa pamoja unahusisha kuundwa kwa bunge la mpito lenye wanachama 90, wakiwemo wawakilishi 10 kutoka upande wa jeshi, 40 kutoka upinzani na wawakilishi 30 kutoka makundi ya kiraia. Viti vyengine 10 vitawachwa wazi kwa vyama vingine vikiwemo vile vya washirika wa zamani wa rais Blaise Compaore ambao hawakushiriki katika mazungumzo hayo.

Serikali ya mpito pia imependekezwa ambapo wanachama wake 25 hawataruhusiwa kugombea katika uchaguzi wa urais na ule wa bunge unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka ujao. Kwa sasa Luteni Kanali Issac Zida anayeiongoza kijeshi nchi hiyo ya Burkina Faso ameahidi kukabidhi madaraka kwa kiongozi wa utawala wa kiraia.

Mazungumzo ya awali Burkina Faso yaliohudhuria na Rais wa Ghana John Dramani Mahama
Mazungumzo ya awali Burkina Faso yaliohudhuria na Rais wa Ghana John Dramani MahamaPicha: AFP/Getty Images/I. Sanogo

Luteni Kanali Isaac Zida alijitangaza kiongozi wa nchi hiyo tarehe mosi Septemba baada ya Blaise Compaore kujiuzulu na kukimbilia Cote d Ivore mwezi uliopita, kufuatia maandamano makubwa dhidi ya juhudi zake, za kubadilisha katiba ili awanie tena urais katika uchaguzi wa 2015 baada ya kukaa madarakani kwa miaka 27.

Taifa hilo la Afrika Magharibi liko katika shinikizo ya kurejesha utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo au ikumbwe na vikwazo vya Kimataifa. Awali Umoja wa Afrika ulio na wanachama 54 ulitoa wiki mbili kwa jeshi la nchi hiyo kurejesha madaraka kwa raia au iadhibiwe kwa kuekewa vikwazo.

Jumuiya ya ECOWAS yaomba vikwazo visifikiriwe kwa sasa

Hata hivyo Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS iliitolea wito jamii ya Kimataifa kutoiwekea Burkina Faso vikwazio kutokana na juhudi za upatanishi zinazoongozwa na rais wa Senegal Macky Sall.

Huku hayo yakiarifiwa wiki iliopita Marekani ilisema bado haijatambua hatua ya jeshi kuchukua madaraka kama mapinduzi kwa kuwa hali hiyo itaifanya Marekani kukatiza mara moja msaada wake wa kijeshi nchini humo.

Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz
Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel AzizPicha: Kenzo Tribouillard/AFP/Getty Images

Kwa sasa Mkuu wa Umoja wa Afrika ambaye ni rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz, yuko ziarani mjini Ouagadougou kulishinikiza jeshi kukabidhi madaraka siku 10 baada ya Blaise Compaore kuondolewa madarakani.

Akiwa uhamishini huko Cote d Ivore, Compaore ameushutumu upinzani na jeshi kupanga mapinduzi dhidi yake. " Walinitaa niondoka, nimeondoka. Historia itatuambia iwapo walikuwa sawa kufanya hivyo," alisema Blaise Compaore aliye na miaka 63 alipokuwa akihojiwa na chombo kimoja cha habari nchini Cote d Ivoire.

Mwandishi Amina Abubakar/Reuters/ AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman