1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kusitisha mapigano Syria waonyesha matumaini

1 Machi 2016

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier na mwenzake wa Marekani, John Kerry wamesema makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Syria yanaonyesha ishara ya matumaini na yanaendelea kuheshimiwa.

https://p.dw.com/p/1I4c4
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/S. Thew

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye wizara ya mambo ya nje ya Marekani mjini Washington, baada ya mkutano wake na Steinmeier, Kerry amesema ni wazi siku zijazo zitakuwa muhimu katika kutathmini kama wanaweza au hawawezi kuongeza kasi kuelekea kupunguza ukubwa wa mzozo wa Syria. Amesema hilo ndilo lengo na wanazingatia vizingiti vilivyoko mbele yao.

''Ukweli ni kwamba tunahitaji kuzuia mzunguko wa mapigano na umwagikaji wa damu unayoiangamiza Syria. Ni rahisi hivyo na tusifanye makosa, kwani njia ya kidiplomasia ndiyo njia sahihi inayoweza kuyaangamiza makundi ya kigaidi kama vile Dola la Kiislamu na Al-Nusra Front na baada ya muda fulani kuwa na Syria imara na iliyo na umoja,'' alisema Kerry

Kwa upande wake Steinmeier amesema tangu kufanyika kwa mkutano wa usalama wa Munich katikati ya mwezi Februari, hatua imepigwa kwenda mbele na wanachozingatia kwa sasa ni kuhakikisha lengo la kusitisha mapigano linakuwa la muda mrefu, ili kuwaruhusu waanze mazungumzo ya kupata suluhisho la kisiasa katika mzozo wa Syria.

Jumuiya ya kimataifa inapaswa kupata suluhisho

Steinmeir alisisitiza, ''miaka mitano iliyopita ya vita vya wenyewe kwa wenyewe watu 250,000 wameuawa, majaribio mengi yameshindikana kumaliza vita vya Syria. Hatupaswi kulalamika, jumuiya ya kimataifa inapaswa kujitahidi kupata suluhisho.''

Watoto wa Syria wakicheza nje wakati mpango wa kusitisha mapigano ukiendelea
Watoto wa Syria wakicheza nje wakati mpango wa kusitisha mapigano ukiendeleaPicha: picture-alliance/dpa/M. Badra

Wanadiplomasia hao wawili wameelezea matumaini yenye tahadhari kuhusu suala la kusitisha uasi, licha ya kuwepo ripoti za matukio kadhaa ya ukiukwaji wa mpango wa kusitisha mapigano. Kerry amethibitisha pande zote zinazopambana nchini Syria huenda zimekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

Amesema kikosi kazi kinachoongozwa na Marekani na Urusi kinachunguza madai yote yaliyokiukwa na kwamba amezungumza na waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov kwa njia ya simu na wote wawili wamekubaliana kuufanya mpango huo ufanikiwe na sio kutafuta njia za kuukwamisha.

Hata hivyo, Kerry amesisitiza kwamba Urusi na Marekani zimekubaliana kutoyajadili madai hayo hadharani. Amesema wakati juhudi zinafanywa kuanza kuyachunguza madai hayo, kwa sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba yatazorotesha mpango wa amani wa kusitisha mapigano.

Wakati huo huo, afisa mwandamizi wa kundi kuu la upinzani nchini Syria linalojulikana kama Kamati Kuu ya Majadiliano-HNC, linaloungwa mkono na Saudi Arabia amesema mpango wa kusitisha makubaliano uko katika hatari ya kuvunjika, kwa sababu mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya serikali yanakiuka makubaliano hayo.

Ama kwa upande mwingine, misaada ya kwanza ya kibinaadamu imeanza kuwasili kwenye maeneo yanayohitaji msaada, tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa kusitisha mapigano, kama sehemu ya juhudi zilizofikiwa kujaribu kuimarisha mpango huo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, RTR,AFP
Mhariri: Josephat Charo