1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa makombora ya ulinzi wazusha zahma barani ulaya

4 Juni 2007

Rais George Bush wa Marekani wiki hii anatarajiwa kuzuru Jamuhuri ya Czech na Poland katika mkakati wa kidploamsia wa Washignton kuhusu kuwashawishi viongozi wa maeneo ya Ulaya Mashariki juu ya umuhimu wa makombora ya ulinzi, hatua ambayo imezusha mgawanyiko katika nchi za Ulaya.

https://p.dw.com/p/CHDH
Rais George W Bush wa Marekani
Rais George W Bush wa MarekaniPicha: AP

Mpango huo wa makombora ya ulinzi unaolenga kuzikinga nchi za magharibi kutokana na mashambulio ya makombora kutoka kwenye nchi sugu kama vile Iran na Korea kaskazini utakuwa na sehemu mbili kufikia mwaka 2011.

Mpango huo unaazimia kuweka kituo cha Radar katika Jamuhuri ya Czech na vifaa vya ulinzi dhidi ya makombora nchini Poland.

Huku mpango huo wa Marekani ukizidi kukabiliwa na upinzani mkali kutoka Urusi, Washington imeahidi kuongeza juhudi za kidiplomasia kati yake, Urusi na nchi wanachama wa jumuiya ya NATO.

Moskow inapinga mpango huo wa Marekani kwa kusema kuwa unalenga kitu kisichokuwepo Urusi pia imesema kuwa Iran na Korea Kaskazini hazina uwezo wa kutengeneza silaha za kinyuklia zitakazo tishia bara Ulaya pamoja na Marekani.

Austria, Ufaransa, Ujerumani, Norway, Ugiriki, Ubelgiji, Netherlands na Luxembourg zimeonyesha kuwa haziafikiani na mpango huo wa Marekani ambao unaungwa mkono na serikali za Jamuhuri ya Czech na Poland.

Watalaamu wameashiria kuwa huenda bara Ulaya linatumbukia katika mgawanyiko mpya kama ilivyokuwa wakati wa uvamizi wa Irak ulio ongozwa na Marekani.

Umoja wa nchi za ulaya kwa mara nyingine tena unakabiliwa na mgawanyiko baina ya nchi wanachama zinazotaka kuwa na uhuru zaidi katika sera zake za nje na za ulinzi na zile nchi zinazopinga Marekani kujiingiza katika sera za ulinzi za bara Ulaya.

Pedro Courrela mchambuzi kutoka taasisi ya maswala ya kimataifa yenye makao yake mjini Lisbon nchini Portugal amesema kwamba azma ya kutaka kuwepo mazungumzo yatakayo zihusisha nchi nyingi ni jaribio la kutafuta uhusiano na nchi nyingi badala ya uhusiano wa pande mbili uliopo sasa.

Marekani haiko tayari kujadili maamuzi yaliyoafikiwa na Jamuhuri ya Czech na Poland. Mchambuzi Courrela amesema itabidi tusubiri iwapo nchi za magharibi zitalileta swala hilo katika mfumo wa makombora ya ulinzi wa NATO.

Ikizingatia wasiwasi wa bara ulaya Jamuhuri ya Czech imeitaka Marekani ifikirie juu ya kutangamanisha mpango wake na mpango wa baadae wa makombora ya ulinzi wa NATO.

Poland inapendelea mazungumzo ya pande mbili tu bila ya kuihusisha Urusi.

Kinyume na rais Vaclav Klaus wa Jamuhuri ya Czech ambae alikutana na rais Vladmir Puttin wa Urusi mwezi Aprili mjini Moskow, na katika hotuba kwa waandishi wa habari rais Klaus alimuhakikishia rais Puttin kuwa vituo vya rada vitakavyowekwa nchini mwake havitakuwa tishio kwa Urusi.

Lakini maoni ya wengi katika miji ya Prague na Warsaw ni kwamba vituo hivi vinatoa fursa kwa nchi hizi mbili kuwa washirika wa Marekani kwa ajili ya kuepukana na ushawishi wa Urusi katika eneo la Ulaya ya Mashariki.

Urusi imesema kuwa inachukuwa tahadhari kuhusu uwezekano wa mashindano mapya ya silaha na imetishia kujiondoa kutoka kwenye mkataba wa matumizi ya makombora ya masafa ya kadiri na yale mafupi na pia imetishia kuwa huenda haitaongeza muda wake wa mkataba wa kupambana na matumizi ya makombora hayo baada ya kumalizika mwaka 2009.

Kuna hofu kubwa kuwa Urusi inaweza kulipiza kisasi kupitia sera zake za uchumi, kwani Jamuhuri ya Czech na Poland zinategemea sana nguvu za nishati kutoka Urusi hivyo basi Moskow inaweza kuzitumbukiza nchi hizi katika mzozo kwa kuzibania nishati.