1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wa Ebola Kongo unaweza kudhibitiwa-WHO

19 Mei 2018

Shirika la Afya Ulimwenguni-WHO, limesema mripuko wa Ebola DRC si kitisho kwa dunia, kwa sababu unaweza kudhibitiwa ndani ya nchi hiyo. Awali ugonjwa huo ulithibitishwa katika jiji la Mbandaka na kuzidisha wasiwasi.

https://p.dw.com/p/2xw9a
Ebola-Ausbruch im Kongo
Picha: Reuters/J. R. N'Kengo

Wataalamu wa  Shirika la Afya Ulimwenguni WHO wamesema mripuko wa maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaweza kudhibitiwa, na hauwezi kuwa kitisho kwa nchi nyingine duniani. Awali shirika hilo lilithibitisha kuwa watu watatu wameambukizwa virusi vya Ebola katika jiji la Mbandaka lenye wakazi milioni 1.5, na kuonya kuwa mripuko huo ungeweza kuwa kitisho kikubwa kwenye kanda nzima.

Wizara ya Afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilisema maambukizi hayo yaligunduliwa katika kitongoji cha Wangata pembeni mwa mto Kongo, katika jiji la Mbandaka. Mripuko huu ni wa tisa kutokea nchini Kongo tangu kugunduliwa kwa maradhi ya Ebola mnamo miaka ya 1970.

Wataalamu wa WHO wamesema hatua za haraka zimeweza kuzuia kuenea kwa mripuko huu mpya uliotangazwa siku 10 zilizopita, na ambao tayari umeuwa watu wasiopungua 25.Wizara hiyo imesema mtu mmoja pekee ndiye aliyethibitishwa kufariki dunia ingawa kuna madai kwamba watu 25 wamefariki.

Visa 44 vya homa ya kuvuja damu vimerekodiwa

Kuzuka kwa Ebola kunasababisha kujaribiwa kwa chanjo mpya ya Ebola ambayo ilionekana kufanya kazi vyema Afrika Magharibi miaka michache iliyopita. Zaidi ya vipimo 4,000 vya chanjo hiyo vimewasili nchini Congo wiki hii huku vipimo zaidi vikitarajiwa kufika. Changamoto kuu itakuwa kuiweka chanjo hiyo katika hali ya baridi katika eneo ambalo lina miundo mbinu duni na umeme katika sehemu chache.

Kongo Ebola Impfstoff in Kinshasa
Chanjo ya Ebola ikiingia nchini CongoPicha: Reuters/K. Katombe

Julien Raickman ni Mkuu wa Madaktari wasio na Mipaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

"Tulijua jana kwamba kumethibitishwa kisa kimoja baada ya uchunguzi wa maabara katika mji wa Mbandaka. Kuanzia mwanzo wa kuzuka kwa maradhi haya," alisema Raickman. "Tumerekodi visa 44 vya homa ya kuvuja damu. Na ni homa ambayo tuliiona, visa vyote vitatu vya Ebola ambavyo vimethibitishwa," aliongeza Mkuu huyo wa MSF.

WHO itaita kikao cha wataalam wa kamati ya dharura baadae leo

Jambo ambalo linadhibitiwa lisitokee kwa sasa ni kuzuka kwa Ebola katika mji wa Kinshasa, mji wenye mamilioni ya watu ambao wengi wao wanaishi katika nyumba za mabanda zisizo na mfumo wa kutoa maji machafu.

Kongo Ausbruch von Ebola
Watu wengi Congo wanaishi katika mitaa ya mabanda isiyo na hali bora ya usafiPicha: Getty Images/AFP/D. Minkoh

Baadae leo, WHO itaita kikao cha wataalam wa Kamati ya Dharura kutoa ushauri kuhusu njia za kimataifa za kulikabili janga hilo na iamue iwapo itabuni mpango wa dharura wa kushughulikia wasiwasi wa kimataifa kuhusiana na Ebola.

Tangu mwaka 1976, huu ni mlipuko wa tisa wa Ebola nchini Congo. Virusi vya ugonjwa huu vinasambazwa kwa watu kutoka kwa wanyama wa porini wakiwemo popo na tumbili. Hakuna tiba maalum ya Ebola. Dalili zake ni homa, kutapika, kuharisha, maumivu ya misuli na wakati mwengine kuvuja damu ndani na nje ya mwili. Ebola inaweza kusababisha vifo katika asilimia 90 ya visa.

Mwandishi/Jacob Safari/Reuters/DPAE/APE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo