1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wa kujitowa muhanga watokea Instabul

19 Machi 2016

Watu watano akiwemo mripuaji wa kujitowa muhanga wameuwawa Jumamosi (19.03. 2016) katika shambulio linalotuhumiwa kufanywa na wanamgambo wa Kikurdi katika wilaya kuu ya utalii na maduka mengi katikati ya mji wa Istanbul.

https://p.dw.com/p/1IGLM
Polisi ya Uturuki yazingira mtaa wa Istiklal kufuatia mripuko Instanbul (19.03.2016)
Polisi ya Uturuki yazingira mtaa wa Istiklal kufuatia mripuko Instanbul (19.03.2016)Picha: picture-alliance/dpa/T. Bozoglu

Mripuko huo wa kujitowa muhanga ambao ni wa nne nchini Uturuki mwaka huu umetokea katika mtaa wa Istiklal eneo kubwa la njia ya waendao kwa miguu ilioambatana na maduka ya kimataifa na ofisi zndogo za ubalozi wa nchi za kigeni mita chache tu kutoka mahala ambapo kwa kawaida polisi huegesha mabasi yao.

Afisa wa mwandamizi wa Uturuki ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba uchunguzi wa awali unadokeza kwamba chama kilichopigwa marufuku cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) au kitengo kinachohusiana nacho kimefanya shambulio hilo.

Afisa huyo amesema mshambuliji huyo aliripuwa bomu kabla ya kufika shabaha yake kutokana na kuwahofia polisi na kuongeza kwamba alikuwa amepanga kujiripuwa katika eneo lenye watu wengi zaidi.

Wageni miongoni mwa majeruhi

Polisi wenye silaha waliuzingira mtaa huo wa maduka ambapo magari kadhaa ya kubebea wagonjwa yalikuwa yamekusanyika.Helikopta za polisi zilikuwa zikizunguka juu ya anga la eneo hilo na watu walikuwa wakikimbia kwa hofu kwa kujipenyeza kwenye vichochoro pembezoni mwa mtaa huo.

Vikosi vya usalama mjini Ankara.
Vikosi vya usalama mjini Ankara.Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Gavana wa mji huo Vasin Sahin amesema mripuko huo umetokea nje ya ofisi ya serikali ya mitaa wakati waziri wa afya Mehmet Muezzinoglu amesema watu 36 wamejeruhiwa katika shambulio hilo wakiwemo wageni 12.

Waziri huyo hakufafanuwa juu ya uraia wa wageni waliojeruhiwa lakini shirika la habari la kibinafsi la Dogan limesema takriban raia watatu wa Israel ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa wakiwemo watoto wawili.Nayo talevisheni binafsi ya NTV imesema raia mmoja wa Iran ni miongoni mwa majeruhi.

Wengi wabakia nyumbani wakihofia usalama

Mtaa wa Istiklal ambao kwa kawaida umechangamka na watu waliofurika kwa manunuzi ya mwishoni mwa juma leo ulikuwa tulivu kuliko ilivyo kawaida kutokana na kwamba watu wengi wamebakia majumbani kufuatia mfululizo wa mashambulizi yaliosababisha maafa.

Mmojawapo wa wahanga wa shambulio la Ankara la mwezi wa Machi.
Mmojawapo wa wahanga wa shambulio la Ankara la mwezi wa Machi.Picha: picture-alliance/dpa/S.Suna

Mripuko wa kujitowa muhanga kwa kutumia gari umeuwa watu 37 mjini Ankara mwezi huu. Mripuko kama huo mwezi uliopita umeuwa watu 29 katika mji mkuu huo wa Uturuki.Kundi la wanamgambo wa Kikurdi limedai kuhusika na miripuko hiyo yote miwili.

Mwezi wa Januari mshambuliaji wa kujitowa muhanga ameuwa takriban watu 10 wengi wao wakiwa ni watalii wa Kijerumani katika kitovu cha historia mjini Istanbul ambapo serikali inalilaumu kundi la Dola la Kiislamu kwa kuhusika.

Uturuki ambayo ni mwanachama wa Jumuiya Kujihami ya NATO inakabiliwa na vitisho vingi vya usalama.Ikiwa kama sehemu ya ushirika unaoongozwa na Marekani nchi hiyo inapambana na kundi la Dola la Kiislamu katika nchi jirani ya Syria na Iraq. Pia inapambana na wanamgambo wa PKK wa chama cha wafanyakazi cha Kurdistan kusini mashariki mwa nchi hiyo ambapo usitishwaji wa mapigano wa miaka miwili na nusu umesambaratika mwezi wa Julai mwaka jana na kutibua matumizi ya nguvu mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea miaka ya 1990.

Vitendo vya kinyama

Waziri wa Afya wa Uturuki Mehmet Muezzinoglu amesema "Sisi kama taifa kwa bahati mbaya hivi sasa tunakabiliana na ana kwa ana na hali isiokuwa na kikomo,vitendo visivyopimika ambavyo ni vya kinyama vyenye kukana maadili ya kibinadamu na vya usaliti."

Gari likiteketea kufuatia shambulio la Ankara.
Gari likiteketea kufuatia shambulio la Ankara.Picha: Reuters/M. Ozer

Katika kampeni yake ya matumizi ya silaha PKK kihistoria imekuwa ikishambulia vikosi vya usalama moja kwa moja na kusema kwamba haiwalengi raia katika mashambulizi hayo.Hata hivyo kutokana na mashambulizi yao ya hivi karibuni inaonyesha kwamba imekuwa ikibadili mbinu.

Uturuki imeimarisha usalama mjini Ankara na Istanbul kuelekea tamasha la Newroz la majira ya machipuko hapo Machi 21 ambapo Wakurdi nchini Uturuki kwa jadi wamekuwa wakilitumia kuyakinisha utambulisho wao wa kikabila na kudai haki zaidi.

Ubalozi mdogo wa Ujerumani ulioko katika wilaya ulikotokea mripuko umefungwa siku za hivi karibuni kwa sababu ya wasi wasi wa kiusalama.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP

Mhariri : Yusra Buwayhid