1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya maneno vyachacha kati ya Saudi Arabia na Iran

24 Novemba 2017

Mrithi wa kiti cha ufalme cha Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, amemwita kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei, kuwa "Hitler mpya wa Mashariki ya Kati katika mahojiano na jarida la New York Times jana Alhamisi

https://p.dw.com/p/2oB4n
Saudi Arabien Mohammed bin Salman Kronprinz mit Macron in Riyadh
Picha: Reuters/Saudi Press Agency

Katika kile kinachoonekana kuwa muendelezo wa vita vya maneno baina ya dola mbili zenye nguvu zaidi kwenye eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati, mrithi wa kiti cha ufalme cha Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, amemwita kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei, kuwa "Hitler mpya wa Mashariki ya Kati" katika mahojiano na jarida la New York Times yaliyochapishwa jana Alhamisi. 

Mohammed bin Salman, ambaye pia ni waziri wa ulinzi wa taifa hilo la kifalme lenye utajiri wa mafuta na mshirika mkubwa wa Marekani, amependekeza haja ya kukabiliana na dai la kujitanua kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Khamenei.

Saudi Arabia, taifa la madhehebu ya Sunni, na Iran inayofuata madhehebu ya Shia, zimekuwa na uhasama mkubwa zikijihusisha na pande tofauti katika vita na mizozo ya kisiasa katika eneo lao la Ghuba na Mashariki ya kati kwa jumla.

Libanon Premier Hariri zeigt sich in Öffentlichkeit
Picha: Reuters/M. Azakir

Hali ya wasiwasi ilizidi mwezi huu, wakati waziri mkuu wa Lebanon mwenye mafungamano na Saudia, Saad Al Hariri, alipojiuzulu katika tangazo la televisheni kutoka Riyadh, akieleza kuwepo kwa ushawishi wa Iran kwa kundi la Hizbullah nchini Lebanon na kitisho dhidi ya usalama wa maisha yake binafsi kuwa ndio sababu za hatua hiyo.

Kwa upande wake, Hizbullah iliitaja hatua ya Hariri kuwa ni kitendo cha vita kilichoandaliwa na maafisa wa Saudia Arabia, dai ambalo Wasaudi wamelikanusha. Hariri alirejea Lebanon wiki hii na kufuta hatua ya kujiuzulu kwake.

Mohammed bin Salman ameliambia gazeti hilo la New York Times na hapa namnukuu: "Tumejifunza kutoka Ulaya kwamba kuvumilia tu hakuna maana. Hatutaki kuwa na Hitler mpya nchini Iran kurejelea kwenye Mashariki ya Kati kile ambacho kilitokea barani Ulaya," mwisho wa kumnukuu.

Hata hivyo, Saudi Arabia yenyewe imekuwa ikifanya mashambulizi kadhaa ya ndege katika vita vya miaka miwili na nusu hivi sasa nchini Yemen kwa lengo la kuwashinda waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran na ambao wanaidhibiti sehemu kubwa ya Yemen.

Mwanamfalme Salman aliliambia jarida la New York Times kuwa wanapata mafanikio katika vita hivyo na kwamba ni wao na washirika wao wenye kuidhibiti asilimia 85 ya ardhi ya Yemen. Kiasi cha watu elfu kumi wameuawa kwenye mzozo huo.

Waasi hao wa Kihouthi walifyetua kombora kuelekea uwanja mkubwa wa ndege wa Riyadh mnamo Novemba 4 jambo ambalo Saudi Arabia ililitaja kuwa ni kitendo cha vita cha Iran.

Katika matamshi mengine makali, Salman alisema mnamo mwezi Mei kuwa Saudi Arabia itahakikisha mapambano mengine yoyote ya hapo baadaye baina yake na Iran yatakuwa ndani ya Iran. Kwa upande wake Khamenei, ameuita ufalme huo kuwa uliolaanika huku maafisa wa Iran wakiishutumu kwa kueneza ugaidi.

Iran Ayatollah Ali Khamenei, Oberster Religionsführer | Gespräch mit Studenten
Picha: Reuters/Leader.ir

Mwandishi: Fathiya Omar/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef