1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaada wa kimaendeleo kwa njia tofauti kabisa!

Josephat Charo29 Oktoba 2007

Mjerumani ambaye ni fundi wa kutengeneza magitaa ya kutumia umeme na aliye maarufu kwa uchezaji wa chombo hicho cha muziki, Peter Coura, aligundua uzuri wa mbao za kiafrika na kujiuliza – kwa nini nisitengeneze magitaa barani Afrika? Amesema na amefanya! Peter Coura anataengeneza magitaa ya kutumia umeme nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/C7rU
Magitaa yakiwa katika maonyesho ya muziki mjini Frankfurt Ujerumani
Magitaa yakiwa katika maonyesho ya muziki mjini Frankfurt UjerumaniPicha: AP

Kwenye bao la kukalia ndani ya karakana moja iliyo kwenye nyumba ya watoto mjini Nairobi Kenya kuna ubao wa mti wa mbambakofi. Na kwa kutumia kifaa maalumu bwana Lucas Barongo anauchonga ubao huo katika muundo unaotakikana. Matokeo tayari yanaweza kuonekana – muundo wa gitaa la kutumia umeme.

´Katika siku chache zilizopita tumetengeneza magitaa 30, saba ya mbambakofi, mawili ya mukangu na moja la mvule.´

Wakati shingo, bweta la sauti na vifaa cha electroniki vitakapowekwa katika gitaa hivi ndivyo ubao wa mbambakofi unavyotoa sauti.

Kinachoendelea katika eneo hili la madongo poromoka la mjini Nairobi Kenya ni jambo jipya kabisa duniani. Gitaa la kwanza la kutumia umeme linalotengenezwa barani Afrika. Mvumbuzi wa wazo hili ni mjerumani Peter Coura. Akiwa anafanya kazi kwa bidii na kwa kujitolea, mzee huyo mwenye mvi anasema.

´Hatimaye hadithi kuhusu gitaa ya umeme ni hadithi ambayo bila muziki wa kiafrika haiwezi kufikiriwa. Muziki wote una vitu vyote vinavyohitajika hapa. Asilimia 85 hadi 90 ya miti ninayohitaji hukua hapa. Na hapa kuna utamaduni wa kazi ya mikono.´

Inaonekana bwana Peter Coura amekaribishwa mjini Nairobi. Kwa miaka 30 iliyopita amekuwa akitengeneza magitaa mjini Frankfurt hapa Ujerumani kwa hiyo ni mmoja wa magwiji wa muziki wa miondoko ya ´Jazz´ na ´Rock´. Lakini alipokalia meza iliyotengenezwa kutumia mbao za mvule kutoka nchini Kenya, bwana Coura hakuweza tena kujizuia.

Peter Coura alisafiri kwa ndege hadi mjini Nairobi Kenya na kuwakusanya maseremala 12 na kubakia katika makazi ya watoto mjini humo. Serema Lucas Barongo anakumbuka.

´Mara ya kwanza nilidhani wanafanya mzaha kwa hiyo sikuwachukulia na uzito wowote. Lakini tulihitaji kutengeneza sampuli ya gitaa kwa sababu pia ilikuwa kazi ya kufurahisha. Hili likiwa somo la kwanza la gitaa maishani mwangu nilifurahia sana pamoja na wenzangu kwenye karakarana kutengeneza gitaa la aina hii.´

Mwanzoni mwa mwaka Peter Coura alisafiri kuja mjini Frankfurt hapa Ujerumani kuleta gitaa linaloitwa Malindi, aina maalumu iliyoundwa na Susan Weinert, mchezaji gitaa la jazz barani Ulaya.

´Muundo wa gitaa la Malindi lina hadithi rahisi sana. Ni la kwanza kutengenezwa, muundo wake ni wa Susan Weinert. Anapenda sauti kutoka mbao ngumu lakini hapendi magitaa mazito.´

Perter Couch anasema kufikia sasa vifaa vya elektroniki huwekwa hapa nchini Ujerumani. Lakini katika siku za usoni mradi wa unaojulikana kwa jina ´Joint Venture´ gitaa zima litakuwa likitengenezwa nchini Kenya. Aidha bwana Couch anasema lengo kubwa ni kuwawezesha maseremala watatu, wanne au watano waweze kujitegemea wenyewe na baada ya kutengeneza magitaa waweze kufanya biashara hii.

Nyumba ya watoto ya SOS ni kama chuo cha kiufundi kinachowafunza vijana kuwa maseremala ili baadaye katika siku za usoni waweze kuanzisha kampuni zao wenyewe. Ni wazo linaloungwa mkono na bwana Lucas Barongo.

Kufikia sasa bwana Peter Crouch ametengeneza aina tatu za magitaa ya kiafrika – Malindi, Masaimara na Samburu. Gitaa aina ya Malindi limetengenezwa katika mfano wa magita ya miaka ya 60.