1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msanii wa Kichina na kampeni dhidi ya pembe za ndovu Kenya

8 Mei 2013

Huku kampeni dhidi ya biashara ya pembe za ndovu zikizidi barani Afrika, mcheza filamu mashuhuri wa China, Li Bingbing, anatembelea hifadhi za wanyamapori za Kenya kuwaelimisha Wachina dhidi ya madhara ya biashara hiyo.

https://p.dw.com/p/18Tst
Patrick Omondi, KWS Head of Species and Conservation Management at a press conference held at UNEP headquarters in Nairobi, Kenya. Copyright: DW/Reuben Kyama
Kenia Patrick Omondi PK UNEP Nairobi 06.05.2013Picha: DW/R. Kyama

Li Bingbing amesema mjini Nairobi kuwa amejitwika jukumu la kuendesha na kueneza kampeini dhidi ya biashara haramu ya pembe za ndovu katika mataifa ya bara Asia.

Katika mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Uhifadhi wa Mazingira (UNEP), Li amesema kuwa raia na wafanya biashara kutoka Uchina wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kupambana na uwindaji haramu wa tembo endapo watachukua jukumu la kutojishirikisha na biashara ya ununuzi na uuzaji wa bidhaa zinazotengezwa kutokana na mabaki ya pembe za ndovu.

Mwanadada huyo wa Kichina aliteuliwa kuwa balozi maalum wa UNEP nchini China mwaka 2010 kutokana na kuwa kwake mcheza sinema hodari aliye na ushawishi mkubwa katika taifa hilo lenye idadi ya watu wengi zaidi duniani.

Mkurugenzi wa UNEP, Achim Steiner, alimsifu Li kwa kipaji chake cha uigizaji akiongeza kuwa kushiriki kwa mwanadada huyo katika harakati za kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu ni kielelezo chema kwa jamii ya ulimwengu kwa ujumla.

"Sababu yetu kuwa hapa na Li ni kwamba yeye kama msanii anayo nafasi ya kuongea na kuwafikia mamilioni ya watu kote duniani kwa kutumia kipaji chake… kwa njia ambayo wengi sisi hatungeweza. Kadhalika miongoni mwa wale anaoshirikiana nao kwenye kampeini hii ni wastadi pia kwenye uwanda huu wa kuhifandi wanyama wa porini," amesema Steiner.

Katika miaka ya karibuni, usalama wa tembo na wanyama wengineo wa porini umekuwamashakani kufuatia kuwepo kwa vitendo vya uwindaji unaofanywa dhidi ya wananya hao.

Pembe za ndovu nchini Kenya.
Elfenbein zur Verbrennung in KeniaPicha: picture-alliance / Robert Hadley

Nchini Kenya kwa mfano, wawindaji haramu hao husafirisha pembe za tembo na kuzipeleka nchi za kigeni kwa ajili ya kuziuza. Uchina ni mojawapo ya masoko makuu duniani yanayofahamika kwa kufanyia biashara haramu ya pembe hizo.

Kulingana na takwimu kutoka kwa Shirika la UNEP, idadi ya tembo wanaowindwa na kuuawa na waharamia katika bara la Afrika imeongezeka maradufu katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita.

Patrick Omondi, mtaalam wa ndovu kutoka Idara ya Wanyamapori nchini Kenya (KWS) anasema kuwa ongezeko kubwa ya mahitaji ya vifaa vinavyotengezwa kutokana na pembe hizo miongoni mwa mataifa ya bara Asia, hasa nchini Uchina na Thailand ni chimbuko la kuenea kwa uwindaji haramu barani Afrika.

Ziara ya mwanaharakati huyo wa Kichina nchini Kenya imedhaminiwa na Shirika la UNEP na shirika lisilo la kiserikali nchini humu la Save The Elephants. Inatazamiwa ziara ya Bi Li nchini Kenya itachangia katika kuwaelimisha mamilioni ya watu nchini China na kwengineko juu ya adhari ya biashara haramu ya pembe za ndovu wanaopatikana barani Afrika.

Mwandishi: Reuben Kyama/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef