1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshahara sawa kwa kazi sawa

P.Martin - (DPA)24 Februari 2009

Tatizo la upungufu wa walimu shuleni,mgogoro wa kampuni ya magari Opel ni baadhi ya mada zilizoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo Jumanne.

https://p.dw.com/p/H0BW

Tutaanza na gazeti la CELLESCHE ZEITUNG. Linasema:

Ni sahihi kwa vyama vya wafanyakazi kusema,tatizo la upungufu wa walimu lililokuwepo hivi sasa,haliwezi kutenzuliwa kwa kuleta msaada kutoka nje. Lakini hilo si pendekezo lililotolewa na Waziri wa Elimu na Utafiti Annette Schavan. Anachotaka waziri huyo ni sekta ya uchumi kuwapa msukumo wanafunzii shuleni.Kwa maneno mengine,wataalamu kutoka sekta zingine hawatochukua nafasi za walimu shuleni bali watasaidia tu kule kuliko na upungufu wa walimu.

Gazeti la WESER-KURIER likiendelea na mada hiyo hiyo linaeleza hivi:

Mwito wa waziri Schavan ni kuwa kila kampuni iwaruhusu wataalamu wake kila juma kwenda kusomesha kwa saa mbili,katika shule zilizopungukiwa na walimu.Hilo bila shaka ni suluhu lisilogharimu pesa nyingi lakini hudhihirisha kuwa baadhi ya wanasiasa wanaamini kazi ya ualimu wala haihitaji kusomewa. Kwa upande mwingine,Schavan vile vile anasema,wale waliofuzu vizuri kidato cha sita yaani Abitur- ndio waruhusiwe kusomea ualimu.Lakini hayo yote si kitu-kilicho muhimu ni kuwa tatizo la upungufu wa walimu shuleni linashughulikiwa.Hatimae umefunguliwa mdahalo kuhusu mustakabali wa shule.

Mada nyingine leo hii inahusika na tofauti ya mishahara kati ya wanawake na wanaume wanaofanya kazi sawa.Gazeti la OFFENBACH-POST limeandika:

Mshahara sawa kwa kazi sawa: Ni aibu kuwa suali hilo linajadiliwa na kuhimizwa karne hii ya 21 katika nchi kama Ujerumani ambako hilo lingekuwa jambo la kawaida tu. Isitoshe,wanaoathirika zaidi ni wanawake wenye watoto au wagonjwa wanaohitaji kusaidiwa nyumbani.Bila shaka hapo wanasiasa na waajiri wanapaswa kutafuta suluhisho.Tatizo hilo limejadiliwa mara nyingi na bado hakuna ufumbuzi uliopatikana.Suali linaloulizwa ni hili:Mpaka lini nchi kama Ujerumani iliyoendelea kiviwanda itamudu kuwatenga wanawake ambao mara nyingi ni wasomi bora zaidi?

Tunamalizia kwa mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari magazetini Ujerumani-mgogoro wa kampuni ya magari Opel inayokabiliwa na hatari ya kwenda muflis.Gazeti la MÜNCHNER MERKUR linasema:

Benki na taasisi za fedha zilizopoteza fedha kwa sababu ya kuchukua hatua za kubahatisha,zinaokolewa kwa kupatiwa misaada mikubwa.Lakini linapozuka suali la kusaidia viwanda serikali inasitasita.Hiyo hudhihirisha kuwa umuhimu wa viwanda hivyo haujatambuliwa.Ukweli ni kuwa kiwanda kinapofungwa si nafasi za ajira tu zinazopotea,bali utaalamu na ujuzi wa wafanyakazi vile vile hutoweka milele.Kimkakati,Ujerumani hakuna kiwanda kilicho muhimu zaidi kuliko sekta ya magari.Ikiwa kampuni ya Opel itatoweka basi hiyo itakuwa balaa.